Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
TANZANIA kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 79 wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM),lenye nchi wanachama 140 kutoka mabara yote Duniani.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 20,2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM),kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Meja Jenerali Francis Mbindi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa mkutano huo ambapo amesema mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wageni 300 kutoka nchi wanachama wa baraza hilo.
Meja Jenerali Mbindi amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika,Jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 12 hadi Mei 19 mwaka huu ambapo utafungiliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kufungwa Mei 17,2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa.
Amesema kuwa Tanzania imepata dhamana kwa mara pili kuwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo toka ulipofanyika hapa nchi,jijini Arusha mwaka 1991 huku akitaja sababu zilizopelekea kuteuliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo kati ya nchi 47 za Bara la Afrika zilizo wanachama wa baraza hilo kuwa ni uwepo wa amani, ulinzi na usalama nchini.
Aidha ametaja lugha tano zitakazotumika kwenye mkutano huo kuwa ni Kiswahili ambapo zingine ni Kiingereza, Kihispania, Kifaransa na Kiarabu.
Pamoja na hayo amesema kuwa kwakuwa mkutano huo ni wa kijeshi hivyo watatoa fursa kwa wageni ya kutembelea maeneo yote yaliyotoa mchango kwa nchinkupata uhuru,ikiwemo mnara wa mashujaa ulipo Mnazi mmoja jiji Dar es Salaam ili kutoa heshima kwa wapigania uhuru wote walioshiriki kupigania uhuru.
“Hata hivyo tutatoa fursa kwa wageni wetu kutembelea vivutio vyetu vya utalii ili tuitangazi nchi yetu,kiutalii,kiuchumi na kibiashara,”amesema.
Baraza hili (CISM) ni shirikisho la kimataifa lililoundwa Februari 18, 1945 baada ya vita kuu ya pili ya dunia na hadi sasa lina nchi wanachama 140 kutoka mabara yote duniani.
Vilvile ametaja lengo la baraza hilo ambalo Tanzania ilijiunga m2aka 1973 kuwa ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani duniani, huku tunu za baraza ikiwa ni kuhamasisha mshikamano, urafiki, heshima, usawa, uadilifu na ushupavu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Michezo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Kanali Martin Msumari amesema kuwa kutakuwa na michezo ya kipaumbele ambayo ni pamoja na riadha, vile vile mchezo wa ngumi na michezo mbalimbali itakuwepo.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu