December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kuuza mbegu nchi yoyote Duniani kupitia TOSCI

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) Patric Ngwediagi ametaja mafanikio ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 kuwa ni pamoja na kupata ithibati ya Kimataifa ya ISTA ambayo imewezesha Tanzania kupata uwekezaji katika biashara ya mbegu na kuuza mbegu nchi yoyote duniani

Ngwediagi ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majuku ya taasisi hiyo kwa mwaka 2023/24 ,mikakati na mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na mafunzo kwa wafanyabiashara wa mbegu 1,832 na kusajili aina 1031 za mbegu.

Aidha amesema taasisi hiyo pia imefanya majaribio ya utambuzi wa mbegu aina 49 na umahiri wa aina mpya za mbegu 18 ,imesajili na kukagua mashamba ya mbegu 1,554,imechukua sampuli 54,000 za mbegu kwa ajili ya vipimo vya maabara lakini pia imetoa lebo za TOSCI milioni 12.3.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Taasisi hiyo imeweza kukagua maghala ya kuhifadhia mbegu 180 na maduka ya mbegu 4,500,imetoa mafunzo ya kuimarisha taaluma za watumishi 45 wa TOSCI na imetoa vibali vya kuingiza mbegu nchini kutoka nje 27,503 na kuuza mbegu aina 1,172 za mbegu.

Kuhusu mafanikio katika usimamizi wa bora wa mbegu kitaifa na kimataifa amesema,kuna ongezeko la mbegu zilithibitishwa ubora wake kitaifa na Kimataifa kwenye mazao ya mahindi ,mpunga,mtama,alizeti,mbegu za maboga,maharage ,pamba,choroko,mbaazi,karanga ,ufuta,ngano,kunde,njugu mawe,ulezi,tumbaku na maharage ya soya.

Pia amesema kuna ongezeko matumizi ya lebo za ubora za TOSCI  na hivyo kupunguza matumizi ya mbegu  feki au zisizo na ubora unaohitajika.

“Lakini pia pamoja na mambo mengine tumepata ithibati ya Kimataifa ya ISTA Mei 2018 ,hii imewezesha nchi yetu kupata uwekezaji katika biashara ya mbegu na kuuza mbegu nchi yoyote duniani ,lakini pia tumejiunga uanachama wa skimu za mbegu za shirika la Kimataifa OECD tangu Desemba 2016 ambapo faida yake ni kuiwezesha nchi kupata uwekezaji katika biashara ya mbegu kwa kuuza nchi yoyote duniani.”

Kuhusu vipaumbele vya mwaka 2023/24,Ngwediagi amesema ni pamoja na kuendelea na uboreshaji wa shughuli za usimamizi wa ubora wa mbegu ,kutekeleza na kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi (AFDP) kwa kuboresha shughuli za udhibiti kwa kujenga maabra ya kuchambua mbegu.

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuthibitisha na kusimamia ubora miche/vipando na pingili za mazao ya miti ya matunda ,migomba na miwa,kuandaa na kutekeleza mkakati wa kuelimisha umma juu ya matumizi ya mbegu zilizothibitishwa ubora na zenye lebo ya TOSCI.