Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
TANZANIA inatarajia kushiriki Mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31 hadi Novemba 2021 nchini Scotland huku ikiweka wazi msimamo wake katika utekelezaji wa Mkataba huo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais ,Muungano na Mazingira Selemani Jafo wakati akitoa tamko kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya mkutano huo.
Amesema katika Mkutano huo, Tanzania itashiriki kikamilifu katika majadiliano ya masuala yenye maslahi mapana kwa nchi yetu na kuweka msimamo wake katika mambo mbalimbali yakiwemo,Rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mkataba na Makubaliano ya Paris kwa mujibu wa Mkataba huo.
“Nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa kiasi cha USD bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2025 ili fedha hizi ziwezeshe nchi zinazoendelea kama Tanzania kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi. “amesema na kuongeza kuwa
“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutoa fedha hizi kama ilivyokubaliwa.
Amesema , Nchi zinazoendelea kama Tanzania ili ziweze kujiimarisha kwa ufanisi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, zinahitaji kujengewa uwezo katika kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Mkataba na Makubaliano ya Paris.
“Msimamo wa Tanzania katika suala hili ni kuzitaka nchi zilizoendelea pamoja na mashirika ya kimataifa kutilia mkazo suala la kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea ili ziweze kutoa mchango wake katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani.”
Amesema msimamo wa Tanzania ni kuwa, sekta ya kilimo isijumuishwe katika sekta zinazotakiwa kupunguza gesi joto kwa kuwa kilimo kinaathirika sana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na kutegemea mvua.
“Kumekuwa na maoni kinzani kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuhusu kujumuisha sekta ya kilimo katika sekta zinazotakiwa kupunguza uzalishaji wa gesijoto…,mchango wa uzalishaji wa gesi joto utokanao na shughuli za kilimo ni mdogo katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea.”amesisitiza Jafo na kuongeza kuwa
“Makubaliano ya Paris yanazitaka nchi zilizoendelea kuziwezesha nchi zinazoendelea kutumia teknolojia mpya na za kisasa ambazo zitasaidia kuongeza uwezo wa nchi hizo kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kupunguza uzalishaji wa gesijoto, kwa kuwa Teknolojia hizo ni ghali na hazipatikani kirahisi. “
“Msimamo mwingine wa Tanzania katika suala hii ni kwamba nchi zilizoendelea zihakikishe nchi zinazoendelea zinapatiwa teknolojia hizo kwa gharama nafuu na kwa uwazi…,makubaliano ya Paris yanaitaka kila nchi mwanachama kuandaa Mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Tanzania iliwasilisha mchango wake kwenye sekretarieti ya Mkataba t 30 Julai 2021. “
Msimamo wa Tanzania katika suala hilo ni kwamba Mkutano huu ufikie maamuzi yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kuwezesha nchi zinazoendelea kutekeleza michango yao na kwamba mapitio ya michango hiyo yafanyike kila baada ya miaka mitano.
Kuhusu Upunguzaji gesijoto kwa kutumia biashara amesema suala la upunguzaji wa gesijoto kwenye uso wa dunia halina budi kufanyika ili ongezeko la joto liwe chini ya nyuzi joto 20C huku akisema, juhudi za ziada zinahitajika ili ongezeko lisivuke nyuzi joto 1.50C kwa ajili ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Makubaliano ya Paris kwenye kipengele cha sita cha makubaliano hayo yanatoa fursa ya nchi mbalimbali kushirikiana kwenye upunguzaji wa gesijoto kwa kutumia mbinu ya biashara…,msimamo wa Tanzania ni kwamba nchi inayouza ziada ya upunguzaji isijumuishe kiwango kilichouzwa kwenye orodha yake ya upunguzaji ili kusitokee kuhesabiwa mara mbili kwani nchi iliyonunua ziada hiyo ndiyo itaweka kiwango hicho kwenye orodha yake ya upunguzaji gesijoto. “
Aidha Jafo amesema jinsi ni suala mtambuka na kwamba halina budi kujumuishwa kwenye mipango na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba uwezeshaji wa wanawake utaleta mafanikio yenye ufanisi mkubwa katika nyanja za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na upunguzaji wa gesijoto.
“Kwa muktadha huu, msimamo wa Tanzania unahimiza utekelezaji wa programu ya miaka mitano kuhusu jinsia na mabadiliko ya tabianchi.”
Aidha amesisitiza kuwa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo ni muhimu kwa vile utaiwezesha Tanzania kufaidika na fursa mbalimbali kama vile upatikanaji wa fedha na teknolojia zitakazosaidia katika juhudi za Serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
“ Hivyo ushiriki wa nchi yetu katika mkutano huo ,unatarajiwa kuleta faida kubwa nchini kwa kupata rasilimali fedha na utaalamu utakaowezesha utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali ya kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini pia utasaidia kufungua uwekezaji wa sekta binafsi na miradi ya Asasi za Kiraia katika miradi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha Waziri Jafo amesema Lengo kuu la Mkataba huo pamoja na masuala mengine ni kuhakikisha kuwa mlundikano wa gesijoto angani zinazosababishwa na shughuli za binadamu unakuwa katika kiwango ambacho hakitaleta madhara kwa binadamu na mazingira.
Amebainisha kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe takriban 3,000 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri na Wataalamu waliobobea katika masuala ya mabadiliko ya tabinchi.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM