December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kunufaika Jumuiya za nishati EAPP, SAPP

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Tanzania inatarajiwa kunufaika na uanachama wake katika jumuiya za nishati za Afrika Mashariki yaani (East African Power Pool) na Kusini (South Africa Power Pool) katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara ya umeme pamoja na kuunganishwa katika gridi ya pamoja.

Hayo yamebainishwa katika warsha ya siku tano iliyowakutanisha wakuu wa sekta ya nishati pamoja na washauri kutoka nchi 13 Afrika katika Hoteli ya Ramada wanaokutana kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya namna ya kuunda kanuni za soko la nishati ya umeme (Market rules) katika biashara ya kuuziana umeme kwenye kanda hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji kutoka TANESCO wakiwa ni shirika mwenyeji linalotoa huduma ya umeme nchini Naibu Mkurugenzi mtendaji usafirishaji umeme Mhandisi Abubakar Issa amesema Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya za nishati za ukanda wa Afrika Mashariki (EAPP) na kusini mwa Afrika (SAPP) ambazo lengo lake ni kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika nchi hizo kwa kuangalia biashara ya kuuziana umeme na uwepo wa gridi ya pamoja.

“Tanzania tutakuwa na uwezo wa kuuza au kununua umeme katika jumuiya za nishati za Afrika Mashariki na Kusini. Kitendo cha miundombinu yetu itakapokuwa imeunganisha jumuiya zote mbili, tutafaidika na mapato kama nchi. Na hii pia itasaidia kuhakikisha nchi zote za Afrika zinasaidiana katika kuwa na umeme wa uhakika. Hili litakuza uchumi wa Tanzania pamoja na bara letu kwa ujumla kwakuwa umeme ni uchumi” amesema Mhandisi Issa.

Amesema hadi sasa miundombinu inaendelea kuunganishwa na malengo ni kwamba biashara ianze mara tu muunganiko wa miundombinu hiyo itakapokamilika.

“Tunaunganisha ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika mfano sisi na Kenya tayari na kwa sasa hivi tunaendelea na Zambia ambapo kwa upande wa Tanzania tuko tayari, na tutakuwa tayari zaidi pale miundombinu inayoendelea kujengwa itakapokamilika,” ameongeza Mha. Issa.

Aliongeza kuwa kwa sasa Tanzania imeanza kwa kuunganisha nchi za Kusini na Mashariki kisha Kanda za Magharibi na Kaskazini zitakuwa tayari na baadae kuwa na muunganisho wa gridi Afrika nzima ili nchi zote ziweze kuuziana umeme.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nishati ya Afrika Mashariki EAPP, James Wahogo, amesema wanatazama namna Mashirika hayo ya umeme yatatumia kanuni za soko zitakazoafikiwa katika warsha hiyo.

“Baada ya kujadili katika warsha hii zitapelekwa baraza la Mawaziri wa Nishati katika nchi hizi ambao wana mamlaka ya kuzipitisha ili ziwe sheria kamili. Hadi 2027 tunategemea Jumuiya ya Mashariki na Kusini zitakuwa tayari zimeshakamilika ambapo wananchi watafaidika kwakuwa watakuwa watapata umeme kwa bei nafuu.”amesema Wahongo.

Naye, Crispen Zana kutoka Shirika la Maendeleo Afrika AUDA NEPAD yenye lengo la kuwa na gridi inayounganisha nchi zote za Afrika amesema kuna Waafrika takribani milioni 600 wanaishi gizani hivyo faida ya jambo hili ni kuhakikisha upatikanaji umeme unawezekana kwa Waafrika wote.

“Nchi moja ikizalisha umeme mkubwa itauzia nyingine na hii ndivyo itakavyokuwa. Lazima tuangalie mikakati ya kuwasaidia wananchi wetu katika miaka zaidi ya 10 ijayo. Jitihada za kila nchi ni kuwa na umeme ambao unatumiwa na watu pamoja na uchumi kwa ujumla” alibainisha Zana

Kuanzishwa kwa sheria za kuongoza soko la umeme kunatarajiwa kuimarisha hali ya upatikanaji umeme nchini kwa ubadilishanaji wa umeme unaovuka mipaka na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kupitia kusanyiko hili Washiriki watabadilishana maarifa na uzoefu na kufanya maamuzi ya pamoja ili kuunda sheria thabiti za soko zinazolenga kuongoza sekta ya nishati ya Afrika Mashariki.

Warsha hiyo ya siku tano inayoendelea inakutanisha wadau kutoka nchi wanachama za Tanzania, Kenya, Uganda, Misri, Ethiopia, Libya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Sudan, Djibouti, Somalia pamoja na Congo DRC.