Na Penina Malundo,Timesmajiraonline
SERIKALI ya Tanzania imesema kuwa itaendelea kusaidia mipango yote ya kidemokrasia yenye lengo la kukomesha mzozo na machafuko yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Pia imetoa ombi kwa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),kutafuta jitihada za kukomesha machafuko na kuleta amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo,Februari 8,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kilichowakutanisha viongozi na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya EAC na SADC,waliokutana kwa lengo la kujadili na kuangalia hali ya usalama nchini Congo.
“Nchi yangu itaendelea kusaidia mipango yote ya kidemokrasia ili kukomesha migogoro inayoendelea nchini Congo, kuwepo kwetu Dar es Salaam kunatoa fursa ya kuweza kujadiliana ni kwa namna gani tunaweza kukomesha vita na kupunguza madhara zaidi kwa binadamu,” amesema Rais Samia
Amesema Congo ipo SADC bado inaendelea kukabiliwa na migogoro na machafuko ambayo yanaleta madhara makubwa kwa maisha ya binadamu na kuathiri biashara pamoja na uchumi mipakani.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa SADC ambaye pia Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema mkutano huo ni ushahidi wa dhamira yao ya pamoja na kwamba juhudi hizo zinawawezesha kuchukua hatua za haraka ili kusitisha vita katika nchi zao.
“Tunatakiwa kuendelea kushikimana kama tulivyokuwa tunapambana kutafuta uhuru dhidi ya wakoloni, tutumie fursa hii kuwa na suluhisho la pamoja ambalo lina lengo la kukomesha vita na kuleta amani ya kudumu Congo,” amesema Rais Mnangagwa.
Amesema hali tete inayoendelea, migogoro iliyopo na ongezeko kubwa la wahamaji lina madhara makubwa si tu Congo bali katika nchi zingine za EAC na SADC.
Naye Mwenyekiti wa EAC ambaye ni Rais Kenya,William Ruto amesema jitihada zilizofanywa na jumuiya hizo mbili ni kukutana kwa pamoja katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa Congo uliosababisha vifo vya watu, kwa njia ya kidiplomasia.
Amesema kukubaliana kwao ni sasa katika kuchukua hatua na kuwaonea huruma mamilioni ya watu ambao wapo katika hatari ya kupoteza maisha na maendeleo yao ya Kiuchumi.
“Tumeona mamilioni ya watu wakihama makazi yao, mgogoro huo unaonesha athari kwa nchi nyingi hivyo tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia DRC kwa kuwapatia misaada. Mgogoro wa Congo ni tete na unahusisha pande mbalimbali na umedumu muda marefu, tusitumie mabomu katika kupata suluhu tuangalie suluhu jumuishi kwa kuangalia chanzo,” amesema Ruto
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa0180599179643506759843-1024x684.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01469097738430657099538-993x1024.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01416445519677018105370-1024x458.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01401916733756224614505-1024x684.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01421250494235141019504-1024x682.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01448008602605078244228-1024x684.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01435624736482257255509-1024x682.jpg)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa01475182638006560987008-1024x682.jpg)
More Stories
Serikali:Dawa za ARV haziuzwi,zipo za kutosha
Wawili mbaroni kwa tuhuma za wizi waya wa TANESCO
Madiwani Lushoto wameridhia bajeti ya bil 54.6 mwaka 2025/26