January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania Iko tayari kuvutia wawekezaji wa mataifa ya nje

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kuwa Tanzania iko tayari kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kupitia Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2024.

Amebainisha hayo leo Agosti 21, 2024, katika Hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Mkutano huo.

Waziri Mavunde amesema kuwa Mkutano huo utaleta pamoja wadau wa kimataifa katika Sekta ya Madini, Wawekezaji, Watafiti wa Madini, Wachimbaji, Wawakilishi wa Serikali, Viongozi kutoka Mataifa ya kigeni, Wawakilishi na Mabalozi wa nchi mbalimbali kwa pamoja wakilenga kujadili fursa za kipekee za Uwekezaji katika uongezaji thamani madini, uchimbaji na hususan wakati huu ambapo mahitaji ya madini muhimu yanaongezeka duniani.

“Ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba madini yote yanayochimbwa hapa nchini ili kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa, kulinda na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea ukuaji wa teknolojia katika Sekta, kuchochea maendeleo ya jamii na uchumi kwa ujumla” amesema Waziri Mavunde.

Akiweka msisitizo kwenye kaulimbiu ya mkutano huo, wenye kauli mbinu ya’Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi’ Waziri Mavunde amesema Mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la majadiliano ya kina yatakayotoa mwelekeo mpya kwa sekta ya madini nchini, huku ukiibua fursa mpya za uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia.

Vilevile, Waziri Mavunde amesema kuwa, Mkutano huo pia unatarajiwa kuwa fursa ya kipekee kwa washiriki kufahamu Sera za Madini za Tanzania, vivutio vya uwekezaji na mipango ya serikali ya kuboresha mazingira kwa ajili ya kuvuna madini kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema kuwa Mkutano huo utakuwa msingi wa kujenga uwezo na uhamishaji wa teknolojia kupitia majadiliano ya kina ya kitaalamu na mawasilisho ambayo yatatoa mwelekeo mpya kuhusu jinsi ya kuboresha sekta, pamoja na kutafuta fursa mpya za kuongeza thamani ya madini.

“Mkutano huu pia utatoa fursa za uwekezaji kwa kuvutia zaidi kampuni za utafiti, uchimbaji, usindikaji na uongezaji thamani madini, na watoa huduma ili kuchimba na kuongeza thamani madini muhimu na vito vinavyopatikana Tanzania” ameongeza Mbibo

Naye, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema kuwa wao kama Chemba ya Migodi wanaishukuru Wizara ya Madini kwa kuwachagua kushirikiana kwa pamoja katika kuandaa mkutano huo.

“Sisi ndio sauti ya Wawekezaji katika Sekta ya Madini hapa nchini, tunaamini kuwa mkutano huu utatuongezea ufanisi katika namna ya uendeshaji wa shughuli zetu za kila siku na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini, pia kupitia ushirikiano huu tunaamini tutakuwa na Mkutano mzuri mwezi Novemba 2024” amesisitiza Mhandisi Mchwampaka.

Pia, Mkutano huo utaambatana na Usiku wa Madini ambayo ni Maonesho ya Vito yenye lengo la kutangaza utajiri mkubwa wa Tanzania katika madini ya vito sambamba na tukio la kuwatambua Kampuni na Wachimbaji waliofanya vizuri kwa kipindi kilichopo.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi wakuu wa Wizara, watendaji wa taasisi za Wizara, Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nje zao nchini, wamiliki wa Leseni kubwa za uchimbaji Madini,wamiliki wa leseni za kati, watoa huduma migodini na wafanyabiashara wa madini, taasisi za fedha na wadau mbalimbali wa madini.