December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, China kuimarisha bishara ya Mifugo na Uvuvi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amekutana na Waziri wa Forodha kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Yu Jianhua kujadiliana namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara baina ya nchi hizo mbili hususan kwenye sekta za mifugo na uvuvi.

Waziri Ulega amekutana na waziri Jianhua jijini Dar es Salaam mapema leo Agosti 14, 2024.

Akiongea katika mkutano huo, Waziri Ulega amesema kuwa mkutano wao huo ni muendelezo wa mkutano baina ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jiping ambapo walikubaliana masuala kadhaa ya kibiashara baina ya nchi hizo.

“Mkutano wetu wa leo unahusu kufanya majadiliano ya namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara kwenye sekta za mifugo na uvuvi ikiwa ni muendelezo baada ya mkutano baina ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Ji Ping”, amesema

Amesema fursa ya biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi nchini China bado ni kubwa na hivyo wanaendelea kujipanga kutumia kila aina ya fursa hizo kushamirisha biashara ili kuinua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Aliongeza kwa kusema kuwa kupitia mikutano hiyo wanayoendelea kuifanya, Waziri Ulega anatumaini kuwa nchi hizo zitaendelea kutatua changamoto za kibiashara na kuendelea kuboresha ushirikiano kwa mbinu na nguvu zaidi ili wananchi wa pande zote mbili waweze kupata manufaa.

Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa, katika kuhakikisha biashara ya mifugo kutoka Tanzania inaaminika duniani, wamejipanga kufanya Kampeni kubwa ya kuchanja mifugo nchi nzima ili kuiepusha na magonjwa na kuifanya iwe bora kwa biashara ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Forodha wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe.Yu Jianhua amesema mahitaji ya kibiashara ya mazao ya samaki na nyama ni makubwa hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo ili kunufaika nazo.

Waziri wa Forodha wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe.Yu Jianhua akimkabidhi picha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wao wa kujadili namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara baina ya nchi hizo mbili hususan kwenye sekta za mifugo na uvuvi uliofanyika jijini Dar es Salaam mapema leo Agosti 14, 2024.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akipeana mkono na Waziri wa Forodha kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Yu Jianhua muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wao wa kujadili namna ya kuendelea kuboresha ushirikiano na kutanua fursa za kibiashara baina ya nchi hizo mbili hususan kwenye sekta za mifugo na uvuvi uliofanyika jijini Dar es Salaam mapema leo Agosti 14, 2024.