Na Godfrey Ismaely, TimesMajira Online
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Botswana, Dkt.Mokgweetsi Masisi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hiyo hususan katika kukuza biashara na uwekezaji.
Ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais Dkt.Masisi ambaye alianza ziara ya kikazi ya siku mbili hapa nchini kwa mualiko wa Rais Samia.
Rais Samia amesema, Botswana na Tanzania zina uhusiano wa kidugu na kihistoria ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Botswana Hayati Seretse Khama hivyo hakuna sababu kwa nchi hizo kuwa na kiwango kidogo cha biashara ikilinganishwa na ukubwa wa uhusiano wake.
Amefafanua kuwa, mwaka 2018 biashara kati ya Tanzania na Botswana ilikuwa kutoka shilingi milioni 731 hadi shilingi Bilioni 3.5 na kwamba Botswana imewekeza hapa nchini kiasi cha dola za Marekani Milioni 231 zilizoajiri Watanzania 2,128.
Rais Samia amesema, katika kukuza uhusiano huo Tanzania ipo tayari kushirikiana na Botswana katika kuboresha ufugaji, kunufaika na uwekezaji wa madini hususan almasi, kukuza utalii na kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vya Botswana.
Amemhakikishia Rais Masisi kuwa Tanzania italinda uwekezaji wowote kutoka Botswana kwa manufaa ya pande zote mbili na amewasihi wawekezaji kutoka Botswana na kwingineko duniani kuja nchini Tanzania kuwekeza kwa kuwa mazingira ya uwekezaji ni mazuri.
Rais Samia amewataka mawaziri na wataalam wa Tanzania na Botswana kufufua kamati ya kudumu ya pamoja (JPC) ambayo haijakutana tangu mwaka 2009 kukutana haraka iwezekanavyo ili kupitia maeneo yote ya ushirikiano na kuongeza maeneo mapya kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Rais Masisi amemshukuru Rais Samia kwa kumualika kuja hapa nchini, alimpongeza kwa kupokea kijiti cha urais na alimuhakikishia kuwa yupo tayari kumpa ushirikiano wowote atakaohitaji na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Botswana.
Rais Masisi amesema, kutokana na uhusiano mzuri, udugu na urafiki uliopo kati ya Tanzania na Botswana nchi hizo hazina budi kudumisha amani na utulivu ili kutoa nafasi ya kukua kwa uchumi na ustawi wa wananchi wake.
Ameongeza kuwa, Botswana iko tayari kubadilishana uzoefu na Tanzania katika masuala ya madini hususan almasi, ufugaji na utafutaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali.
Rais Dkt.Masisi ameungana na Rais Samia kutaka JPC ikutane ndani ya miezi mitati na alimualika Rais Samia kufanya ziara rasmi nchini Botswana.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato