November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANTRADE: Zingatieni masharti ya masoko

Na Irene Clemence, TimesMajira Online

WITO umetolewa kwa wazalishaji wa bidhaa nchini kuhakikisha wanazingatia masharti ya uuzaji na uzalishaji wa bidhaa zao katika masoko ya nje ili kuteka soko hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) mara baada ya kushiriki katika mkutano wa wadau wa uzalishaji na uuzaji wa bidhaa za nyama, matunda ya parachichi Kaimu Meneja wa Uendelezaji Bidhaa kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Masha Hussein.

Amesema, nchi mbalimbali kutoka nchi za Saudi Arabia, Kuwait,Qatar na Nchi za Falme za Kiarabu, zimeshiriki katika mkutano huo uliolenga kujadili hatua za uuzaji wa bidhaa hizo katika nchi husika.

Amesema, wazalishaji wa bidhaa bado wana elimu ndogo kuhusiana na uzalishaji na namna ya kuweka bidhaa zao viwango vinavyotolewa.

Akitolea mfano amesema, bidhaa hizo zimekuwa hazina vifungashio vyenye taarifa zinazojitosheleza hasa zinapokwenda kuuzwa nje ya nchi.

“Kutokana na changamoto hii tumeona ni muhimu kuanza kutoa elimu mara kwa mara kwa wafanyabiashara hawa ili waweze kujua mbinu mbalimbali za kupambana na kuchangamkia fursa hizi.

“Mwitikio wao wa kijitokeza kuchangamkia fursa hizo ni mkubwa sana, lakini shida huwa inakuja kwenye kutekeleza yale masharti yanayokuwa yamewekwa kwa wauzaji wa bidhaa hizo katika kila nchi husika,”amesema.

Vilevile amesema, licha ya nchi ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo, lakini bado kiwango cha nyama kinachouzwa katika nchi zenye uhitaji ni kidogo kuliko malengo.

“Tanzania sisi tuna mifugo mingi sana, lakini ukiulizwa ni kiwango kinachouzwa kwenye hizo nchi zinazohitaji ni kidogo sana na haijafikia kile kinachohitajika katika nchi hilo,”amesema Masha.