November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tantrade yapongezwa kuboresha mazingira ya biashara

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TANTRADE kwa kuboresha mazingira ya biashara hususani Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) 2023.

Kamati hiyo imeiagiza Tantrade kupitia Sheria na kuwa na mikakati mahususi ikiwemo ya uboreshaji wa miundombinu katika maonesho ya sabasaba na utafutaji wa masoko kwa bidhaa za Tanzania inayoendana na wakati na mabadiliko ya Teknolojia

Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mariam Ditopile (MB) Agosti 15, 2023 wakati ikipokea Taarifa ya Hali Halisi ya Utendaji wa Majukumu ya TANTRADE katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Aidha, wajumbe hao walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali kuhusu uendelezaji wa biashara hususan mauzo ya nje, utafutaji wa masoko, biashara mtandao na mapendekezo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ukuzaji wa biashara

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe(MB) akijumuisha maoni na mapendekezo hayo ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo yatatekelezwa ili kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara, kukuza biashara na mauzo ya ndani na nje na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ameeleza Kamati hiyo kuwa Wizara imeanza kupitia na kurekebisha Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria inayoaimamia Tantrade ili ziendane na wakati na mabadiliko ya teknolojia

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade Latifa Mohamed akiwasilisha taarifa ya Taasisi yake kwa Kamati hiyo, amesema jukumu kuu la Tantrade ni kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje ya nchi ili kuimarisha biashara yenye tija katika maendeleo ya kiuchumi nchini.