Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana na Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) wameingia makubaliano ya ushirikiano katika mradi wa huduma ya usafiri katika kipindi chote cha maonesho ya 46 ya kimataifa Sabasaba (DITF).
Makubaliano hayo yatajumuisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kuwasafirisha washiriki na wahudhuruaji wa maonesho kutoka Kituo cha Gerezani Kariakoo hadi Sabasaba ambapo watasafirishwa kwa mabasi yaendayo haraka.
Hayo yamesemwa leo (Juni 6, 2022) jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Mohamed wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo na DART huku akisema kuwa maudhui ya ushirikiano huo ni kufanya kazi kwa pamoja na kuongeza wigo wa mapato kwa Taasisi zote mbili;
“Ruti ambayo tumetiliana saini leo ni kwa wananchi kutoka gerezani kuletwa hapa kwenye maonesho ya sabasaba ambapo gari halitosimama kituo chochote, litatoka moja kwa moja kwenye maonesho lakini pia wananchi wataweza kukata tiketi katika kituo tajwa cha mwendokasi”
Aidha Mkurugenzi huyo amesema lengo la muda mrefu katika Ushirikiano huo ni kuhakikisha mpaka kufikia 2027 na kuendelea usafiri wa uhakika wa mabasi yaendayo haraka yatakayo rahisisha usafiri kwa washiriki na watembeleaji wa maonesho katika viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere (sabasaba) unapatikana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Edwin Mhede amesema mbali na kuhakikisha watu wanafika kwa urahisi wakitoka gerezani kuletwa sabasaba kwaajili ya maonesho na kuwarudisha pia Gerezani, wataleta huduma ya WiFi hivyo wafanyabiashara wajitokeze kutangaza biashara zao;
“Tutaleta huduma ya bure ya WiFi ili kipindi chote cha maonesho wale watakaokuwa maeneo ambayo hayazidi Mita 20 watapata huduma hiyo lakini pia nawakaribisha wote ambao watakuja kuonesha bidhaa na huduma zao sabasaba, watumie fursa hii ya WiFi kujitangaza”
Dkt. Mhede ameongeza kwa kusema kuwa sekta ya biashara itazidi kushamiri kama endapo itatangazwa hivyo DART na TANTRADE wameleta huduma hiyo kwa kupata watazamaji bure lakini pia kwa watakaoleta matangazo gharama yake itakua ni nafuu.
Amesema wanachokifanya katika maonesho ni mwanzo wa kuianzisha awamu ya pili ya huduma ya mabasi yaendayo haraka ambapo kuanzia mwezi machi 2023 njia ya sabasaba itafunguliwa rasmi na wakazi wa mbagara wataanza kutumia huduma za mwendokasi.
Naye Mwanasheria kutoka DART, Domina Madeli, amesema DART na TANTRADE zinatukuwa na mahusiano ya muda mfupi na muda mrefu;
“Mahusiano ya muda mfupi ni haya yanayokwenda kuanza tarehe 27 Juni 2022 hadi tarehe 14 Juni mwaka huu ambapo ni utoaji wa huduma za usafiri kutoka vituo Vilivyohainishwa kuletwa sabasaba”
“Mahusiano ya muda mrefu ni pamoja na huduma ya maegesho kwa mtumiaji wa mfumo wa DART awamu ya pili pamoja na watumiaji wa sabasaba, ubia katika utekelezaji wa mradi wa maendelezo yatajayokuwa na maboresho ya usafiri wa Umma lakini pia usanifu na uboreshaji wa eneo la sabasaba”
Kwa upande wake mwanasheria kutoka TANTRADE, Emma Msofe amesema kuwa makubaliano hayo yatawawezesha wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali yaliyopo Dar es salaam na popote anapoishi kufika katika maonesho kwa urahisi kwasababu mabasi hayo ya DART yatawachukua na kuwaleta hadi eneo husika.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua