December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yasaidia vifaa tiba Hospitali ya Bombo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Tanga

SHIRIKA la Umeme Tanzanoa TANESCO, jana imetoa msaada wa vifaa tiba kwenye wodi ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, vyenye thamani ya sh. milioni nne kwa ajili ya kuwasaidia watoto.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa hivi karibuni na Mshauri Mkuu wa shirika na Katibu wa Sheria wa TANESCO, Wakili Amosi Ndegi kwa Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Beatrice Rimoy.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Wakili Beatrice amesema wameona kuna haja ya kutoa msaada wa vifaa tiba kwa watoto kwenye hospitali hiyo ikiwa ni sehemu yao ya kurudisha kwa jamii.

“Tumeona ipo haja ya kutoa msaada huu wa vifaa tiba kwa watoto kwenye hospitali hii kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na tuna imani, vitatumika kama ilivyokusudiwa,” amesema.

Amesema kwa kawaida shirika hilo limekuwa na utamaduni wa kufanya mikutano ya kiidara, au watu wenye taaluma moja wanaofanya kazi pamoja kwenye shirika kipindi hiki, wapo Tanga wao kama Idara ya Ukatibu wa Sheria inayohusisha wanasheria na Maofisa Usalama wa TANESCO, lengo ni kufanya tathmini ya malengo waliokuwa nayo katika utendaji wa shughuli za kawaida za kila siku kwenye shirika hilo mwaka mzima.

“Tupo hapa Tanga wiki nzima tukijadili mafanikio na changamoto, ili kupata namna nzuri ya utendaji kuboresha huduma inayotolewa na TANESCO kwa jamii, watu wengi wanadhani ni shirika la kibiashara lakini hapana, tupo kuhudumia zaidi na ndiyo maana leo (jana) tupo hapa tukiwezesha huduma ya watoto hospitalini.

“Lakini pia hata bei ya umeme vijijini, sasa ni 27,000 badala ya sh. 300,000 na hii pia ipo kihuduma zaidi, kuhakikisha wananchi wote wanamudu gharama za kuunganisha umeme,” amesema.

Amesema pia wanaziangalia changamoto zinazowakabili ili kutafuta majibu na utatuzi wake kwa lengo la kurahisisha na kuboresha mazingira na ari kwa watendaji walionao.

“Lengo letu kubwa kuwepo hapa ni kwamba tulikuwa na jukwaa la Idara ya Katibu wa Shirika, ambayo hukutana kila mwaka kuzungumzia tathmini na changamoto za utendaji kazi zetu ndani ya shirika na kwa kuhitimisha kikao chetu leo (jana), TANESCO kama sehemu ya jamii tumeona ipo haja ya kutoa msaada wa vifaa tiba kwa watoto Hospitali ya Mkoa wa Tanga Bombo,“ amesema.

Awali akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Ofisa Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Tanga Beatrice, ameishukuru TANESCO kwa msaada huo ambao ulikuwa ni uhitaji mkubwa wa watoto.

Amesema na mahitaji yao yamegawanyika kwenye maeneo matatu ikiwemo watoto wadogo waliozaliwa chini ya mwezi mmoja, waliozaliwa ambao hawajafika mwezi mmoja, wana wodi ya watoto wa mwezi mmoja mpaka miaka 10 ikiwemo watoto wenye magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kuambukiza, kuharisha na matumbo hivyo msaada huo utasaidia kuwahudumia watoto hao.

Naye Daktari wa wodi ya watoto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Dkt. Tumaini Mchiiyo amelishukuru shirika hilo kwa kuwapa vifaa ambavyo vitawasaidia watoto wenye changamoto mbalimbali na hivyo, kuwezesha watoto kupata tiba iliyoboreshwa zaidi wawapo hospitalini.