December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yaanza awamu ya pili ya maandalizi ya kupokea umeme kutoka bwawa la umeme Julius Nyerere

Na Mwandishi wetu

SHIRIKA la Umeme Tanzania(TANESCO),linaanza rasmi utekelezaji wake wa awamu ya pili ya maandalizi ya kupokea umeme kutoka kwenye mitambo yakufua umeme ya bwawa la Julius Nyerere kuingia kwenye gridi ya Taifa.

Upokeaji huo wa umeme unatarajia kuanza rasmi leo Januari 13 hadi 21 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano wa Umma Tanesco, imesema kipindi zoezi hilo litakapoendelea kutakuwa na athari za kutopatikana kwa umeme kwa nyakati tofauti kwa baadhi ya maeneo yaliyounganishwa na Gridi ya Taifa.

Imesema miongoni mwa athari hizo zitakazotokea ni pamoja na  njia ya msongo wa kilovoti 220 Luguruni -Morogoro ambapo  italazimika  kuzimwa na kuiunga kwenye kituo cha 400kV cha Chalinze.

”Kuzimwa  kwa njia hii kutaathiri uwezo wa usafirishaji wa umeme kwenda mikoani na ubora wa umeme kwa mikoa ya pwani na Dar es Salaam kutokana na athari hizi shirika linalazimika kupunguza matumizi ya umeme kwa wateja ili kuendana na uwezo wa njia za usafirishaji na kuwa na uhakika wa ubora wa umeme.”amesema.

Amesema kuhamishiwa kwa njia hii kwenye kituo cha kupoza umeme cha chalinze,sambamba na njia nyingine za usafirishaji umeme zitakazohamishiwa kwenye kituo hicho katika siku za usoni ,kutawezesha kusafirisha umeme unaozalishwa kwenye bwawa la Julius Nyerere na kuufikisha katika maeneo mbalimbali ya nchi .