January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO, Wawekezaji binafsi Ludewa wafikia makubaliano

📌 Ni kuhusu TANESCO kukabidhiwa miundombinu ya kusambaza umeme

📌 Ludewa kujengwa kituo cha Kupokea na Kupoza umeme

📌 Kapinga asema Vijiji 70 kati ya 76 Mbulu vimepatiwa umeme

Imeelezwa kuwa, Serikali na Wawekezaji wanaowauzia umeme wananchi katika baadhi ya kata za Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wamefikia makubaliano ya kisheria ili miundombinu ya usambazaji umeme katika Kata hizo ikabidhiwe kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga leo Juni 26, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mbunge wa Ludewa, Mhe. Zacharius Kamonga aliyetaka kufahamu Serikali itamaliza lini changamoto za bei na mgao wa umeme katika Kata hizo.

Kapinga ameongeza kuwa, hatua zote za makabidhiano zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Julai, 2024 na baada ya kukamilika, TANESCO watabadilisha mita za umeme ili ziendane na mifumo ya TANESCO na kuwawezesha wananchi wa Kata hizo kutumia umeme wa Gridi ya Taifa.

Alitaja Kata hizo kuwa ni Mawengi, Lubonde, Lugarawa, Lupanga, Mlangali, Madilu, Milo na Mawengi ambazo zimekuwa zikipata umeme kutoka kwa Wawekezaji binafsi (JUWUMA na MADOPE HCL.

Kuhusu ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme kujengwa katika Wilaya ya Ludewa, amesema Serikali inaangalia namna bora ya kutekeleza ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kutumia Mpango wa Gridi Imara.

Amesisitiza kuwa, Wananchi wa Ludewa wanahitaji umeme mwingi na wa uhakika kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao vikiwemo viwanda vidogo na vikubwa.

Vilevile amesema kuwa, Serikali kupitia Mkandarasi Ok Electrical inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na tayari mkandarasi ameshafanya upimaji na usanifu wa kina na mwanzoni mwa mwezi Julai 2024 anatarajiwa kuanza kusimika nguzo ili kuziunganisha Kata hizo na Gridi ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Serikali imemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa Usambazaji wa umeme katika Vijiji vilivyopo mwambao wa Ziwa Nyasa, kukamilisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati.

Naibu Waziri Kapinga amesema kuwa iwapo mkandarasi huyo atashindwa kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa, atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo wakandarasi wengine wazembe.

Pia, Kapinga amesema Serikali inaendelea
na usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Mbulu ambapo vijiji 70 kati ya 76 vimeshapatiwa umeme kupitia REA.

Aidha, kazi ya usambazaji umeme katika Vijiji 6 vilivyosalia inaendelea ambapo mkandarasi anafanya kazi ya kuvuta waya na kuweka Mashineumba katika vijiji hivyo.

Pia Mradi wa Ujazilizi utapeleka umeme katika Vitongoji vyote nchini kwa awamu tofauti.