Na Cresensia Kapinga, TimesMajiraOnline,Songea
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeingia makubaliano ya pamoja na wafanyabiashara wa vyuma chakavu mkoani hapa kwa ajili ya kulinda miundombinu mbalimbali iliyojengwa na na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi ikiwemo ya umeme ili isihujumiwe.
Makubaliano hayo yamefikiwa kwenye kikao cha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa vyuma chakavu kutoka wilaya zote za mkoa huo wakiwemo na viongozi wa Jeshi la Polisi na wale wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Kikao hicho kimejadili mkakati wa kupambana na watu wanaohujuma miundombinu ya umeme mkoani Ruvuma ambapo tangu Januari hadi Juni, mwaka huu hali uharibifu wa miundobinu ya umeme imekuwa mbaya na kulisababishia shirika hasara.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Kaimu Meneja wa TANESCO mkoani Ruvuma, Mhandisi Malibe Boniphace amesema wameamua kufanya kikao hicho kwa kuwashilikisha wadau hao baada ya kubaini uwepo wa uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Tanesco na kuisababishia hasara Serikali .
Akizungumzia uhalibifu wa miundombinu ya umeme, Boniphace amesema wamekuwa wakikata nyaya za umeme na vyuma ambapo wateja wakubwa wa vifaa hivyo ni baadhi ya wanunuzi wa vyuma chakavu .
Amesema kikao hicho kitasaidia kushirikiana kuwafichua wahalifu ambao wamekuwa wakiharibu miundombinu hiyo na kuwafanya baadhi ya wananchi kukosa huduma za umeme pamoja na kuisababishia hasara Serikali.
Kwa upande wake mkuu wa Oparesheni Kamishina Msaidizi wa Polisi, ACP Ramia Mganga amesema kuwa jeshi la Polisi lipo imara kupambana na waharifu wa miundombinu hiyo kwa kuwasaka kila sehemu patakapofanyika uharifu .
Mganga ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Marko Chiliya alisema kuwa baadhi ya waharibifu wa miundombinu ya umeme ,maji na ya barabara wameweza kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Amesema kuanzia sasa makubaliano yaliofikiwa na wafanyabiashara wa vyuma chakavu yatasaidia kupunguza uharifuhuo.
Naye Afisa usalama usimamizi kanda ya kusini, Richard Damas amesema vikao hivyo vitafanyika nchi nzima kwa kuwa Serikali karibu kila mkoa kuna miradi mbalimbali inafanyika ikiwemo ya Tanesco .
Naye mmoja wa washiriki wa kikao hicho ,Kadoda Mbalale ambaye pia ni mfanyabiashara wa vyuma chakavu amesema kupitia kikao hicho wamepata uelewa juu ya kujiepusha kununua vyuma chakavu vinavyotokana na miundombinu ya Serikali.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba