Na Nasra Bakari, TimesMajira online
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA) kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya jinsia wamewataka wanajamii kuzuia ukatili wa kijinsia, unyanyasaji na ubakaji kwa watoto unaoendelea nchini .
Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama hicho Dkt.Rose Reuben amesema, TAMWA pamoja na wadau wengine wa masuala ya jinsia wamekuwa wakiimba na kuitaka jamii kuzuia ukatili kwa zaidi ya miaka 30,huku wakililia mabadiliko ya sera, sheria na hata kutoa elimu kwa jamii lakini bado tatizo hili linaendelea.
“Tunahitaji zaidi ya sheria kukomesha ukatili huu, tunahitaji maamuzi magumu kutoka ngazi zote kuanzia familia, wanajamii, viongozi wa dini zote na serikali kwa ujumla wake kwa sababu watoto walio taifa la kesho wanaharibikiwa kimwili na kisaikolojia”, amesema.
Mkurugenzi huyo amesema, taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilitolewa na Jeshi la polisi katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2021 zinazoonyesha mikoa ya kipolisi iliyoongozwa kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 459.
Ametaja makosa yaliongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899 kumpa mimba mwanafunzi 1677, ulawiti 1,114 kumzorotesha mwanafunzi masomo 790, shambulio 350 wakati tukiendelea kutafuta suluhisho la janga hili.
“Utafiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Haki ya Elimu, unaonyesha kuwa watoto wengi hawafundishwi elimu ya afya ya uzazi , lakini zaidi hasa walimu nao wanaogopa kufundisha wanafunzi mada hizo, hapa ndipo mzizi wa tatizo ulipo.
“Ni dhahiri kuwa mambo yanayohusu afya ya uzazi na ukatili wa kingono hayazungumzwi ndani ya familia wala shuleni tena wengine wanaona ni mambo ya aibu yasiyostahili kujadiliwa hivyo yanabaki kuwa masuala ya wadau na serikali ambapo nao husuluhisha tatizo na sio mzizi wa tatizo”, amesema.
Amesema, wakati wakijianda na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ifikapo Agosti 23, ni wakati muhimu kwa viongozi, wazazi, walezi, wasimamizi wa sheria, wadau wa masuala ya jinsia na watoto kujithamini wapi penye mapengo ili tuzibe ombwe hili la ubakaji wa watoto.
Dkt, Reuben amesema TAMWA imesikitishwa na ubakaji huu wa watoto unaoendelea nchini na wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutamka kuwa hili ni janga na kutoa maamuzi magumu kunusuru watoto wetu.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango