November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAMISEMI yaomba tril. 10.125

Na Mwandishi wetu, timesmajira

OFISI ya Rais – TAMISEMI, taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 zimeomba Bunge kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2024/25 yenye jumla ya shilingi trilioni 10.125.

Kwa mwaka 2023/24, Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliidhinishiwa bajeti ya trilioni 9.18, kati ya fedha hizo, trilioni 3.52 ni fedha za maendeleo na trilioni 5.65 ni za matumizi ya kawaida na hadi kufika Machi, 2024 ofisi imekusanya na kupokea trilioni 6.99 sawa na asilimia 76.18 ya fedha zilizoidhinishwa na kati ya hizi trilioni 4.47 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na trilioni 2.52 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha trilioni 2.06 fedha za ndani na bilioni 456.39 fedha za nje.

Haya yamebainishwa leo Aprili, 16, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zake kwa mwaka 2024/25.

Amesema kati ya fedha zinazoombwa, zaidi ya trilioni 6.71 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati zaidi ya trilioni 3.42 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo zaidi ya trilioni 2.27 ni fedha za ndani na trilioni 1.145 ni fedha za nje.

Aidha, Mchengerwa amesema katika mwaka 2024/25, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 imepanga kukusanya maduhuli na mapato ya ndani jumla ya zaidi ya trilioni 1.60 ikilinganishwa na trilioni 1.14 iliyoidhinishwa mwaka 2023/24, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 456.89 sawa na asilimia 39.93.

Amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 188.96 ni makisio ya kodi ya majengo ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI ambayo yatakusanywa na mamlaka za serikali za mitaa zilizopewa uwakala wa kukusanya kodi hiyo na kuwasilisha makusanyo hayo Mfuko Mkuu wa Serikali huku Sh. bilioni 55.42 ni mapato ya ndani ya taasisi wakati Sh. milioni 315.93 ni maduhuli ya mikoa na Sh. trilioni 1.35 ni za mapato ya ndani ya halmashauri.

Mchengerwa amesema pia Sh. bilioni 17.79 zimetengwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024 na kati ya fedha hizo bilioni 8 ni fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya uratibu Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Makao Makuu) na Sh. bilioni 9.79 ni mchango wa halmashauri kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huo.

“Uchaguzi huu utahusu uchaguzi wa viongozi katika ngazi ya msingi ambao ni wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji, wajumbe wa halmashauri ya vijiji na wajumbe wa kamati za mitaa.”

Amesema katika mwaka 2024/25, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi bilioni 357.85 za ruzuku ya fedha za maendeleo za serikali kuu na washirika wa maendeleo katika sekta ya afya.

Waziri Mchengerwa amesema pia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia trilioni 1.02 kupitia ruzuku ya serikali kuu na washirika wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli katika sekta ya elimu huku ikitumia Sh. bilioni 190.57 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi wa mikoa na wilaya, kuendelea na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa ikiwemo majengo ya utawala, ikulu ndogo, makazi ya viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na tarafa katika mikoa 26.