April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAMISEMI yaomba kupitishiwa bajeti ya shilingi Trilioni 11.78

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amelipomba Bunge kuidhinisha skisi cha shilingi Trilioni 11.78  kwa ajili ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI na taasisi zilizo chini yake katika kipindi cxha mwaka wa fedha wa 2025 /2026.

Mchengerwa ametoa ombi hilo Bungeni jijini Dodoma April 16,2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo katyika kipindi cha mwaka 2025 /2026 huku akisema ,kati ya fedha hizo , shilingi trilioni 7.8 ikiwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida yanayojumuisha Mishahara , Matumizi Mengineyo na shilingi trilioni 3.9 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

Waziri huyo ametaja vipaumbele vya ofisi hiyo huku  akiwaelekeza  wakuu wa mikoa kuwasimamia wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kipindi hicho.

Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafikia malengo,kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya afya ya msingi, elimumsingi na sekondari kulingana na mipango iliyowekwa na kuhakikisha mapato katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa yanakusanywa kupitia mifumo ya TEHAMA ya Serikali pamoja na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mifumo hiyo ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.

Vile vile Mchengerwa ametaja vipaumbele vingine kuwa ni Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha inatekeleza Mikakati ya Uchumi wa Buluu, nishati safi ya kupikia na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira.

Pia Mikoa na mamlaka za serikali za mitaa iendelee kuimarisha mifumo stahimilivu na endelevu ya utoaji wa huduma bora za afya, ustawi wa jamii na lishe ili kuboresha huduma ambayo ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Wakuu wa mikoa na wakurugenzi wahakikishe watoto walio chini ya miaka mitano wanajiunga kwenye vituo vya jamii vya kulelea watoto wadogo mchana.

“Aidha, kila halmashauri itapimwa utekelezaji wa vipaumbele hivi kwa kuzingatia miradi iliyotengewa bajeti kwa Mwaka 2025/26.”alisema Mchengerwa

Utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati

Mwaka 2025/26 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi bilioni 44.85 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Amesema,kati ya hizo shilingi 28.75 zitatumika kugharamia miradi mipya 31 na shilingi bilioni 16.10 ni zitatumika kugharamia miradi 19 inayoendelea.

Usimamizi wa mikopo ya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu

Amesema Mwaka 2025/26 shilingi bilioni 123.92 zimetengwa na mamlaka za serikali za mitaa kwa ajili ya utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mchengerwa amesema,kati ya fedha hizo shilingi bilioni 18.35 zitakopeshwa kupitia Mfumo wa Kibenki katika Halmashauri 10 za mfano. Aidha, shilingi bilioni 105.57 zitatolewa kupitia Mfumo wa Serikali Ulioboreshwa kwa halmashauri 174.

Uendelezaji Vijiji na Miji      

Mwaka 2025/26 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi bilioni 32.04 kwa ajili ya uendelezaji wa vijiji na miji.

Amesema,shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kukamilisha mapitio ya muundo wa Mji wa Dar es Salaam uendane na ukuaji wake kijiografia na kiuchumi ili kuwa Jiji Kuu lenye utawala na uendeshaji.

Shughuli nyingine ni kuratibu utekelezaji wa Mpango Kabambe Jumuishi wa Jiji la Kibiashara na Uwekezaji la Kwala, Mkoa wa Pwani na kukamilisha mapendekezo ya rasimu ya Sera ya Maendeleo Vijijini na Mijini.

Aidha Mchengerwa ametaja shughuli zitakazofanyika na Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026 ni pamoja na ujenzi ,matengenezo ,ukarabati wa miundombinu ya barabara na usafiri na usafirishaji wa Vijijini na mijini kupitia Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini (TARURA).

Amesema ,shughuli hiyo imepangwa kutumia kiasi Cha shilingi Trilioni 1.18 ambapo kati ya Fedha hizo shilingi bilioni 257.03 ni za Mfuko wa barabara ,shilingi bilioni 127.50 Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ,shilingi bilioni 325.77 ni za tozo ya mafuta ya oetroli na dizeli ya shilingi 100kwa lita na shilingi bilioni 423.79 ni fedha za nje.

”Kupitia Mfuko wa Barabara; Matengenezo ya barabara kilomita 23,105.78, box kalavati 23, mistari ya kalavati 1,647, Drift 2, na mifereji ya maji ya mvua mita 73,405, barabara za lami kilometa 17, barabara za changarawe kilometa 108.8 na madaraja mawili, Kazi hizi zitafanyika katika wilaya zote 139 Tanzania bara.” amesema

Alisema,Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo kukamilisha taratibu za ununuzi wa mtoa huduma kwa njia ya ubia ya uendeshaji (PPP) wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Kwanza na ya Pili .

Pia wakala huo utaendelea na maandalizi ya usanifu na ujenzi wa miundombinu Awamu ya Tano ya Barabara za Nelson Mandela, Mbagala na Tabata -Segerea – Kigogo zenye urefu wa kilometa 26.0.

Katika eneo hilo alisema,katika mwaka 2025/26, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi trilioni 1.44 za ruzuku ya matumizi mengineyo, fedha za maendeleo za serikali kuu na washirika wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika sekta ya elimu.

Amesema,shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na Ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,402 kati ya hayo 8,057 ni shule za msingi na 345 ni sekondari, matundu ya vyoo 19,095, umaliziaji wa maboma ya maabara 350; mabweni 114 kwenye shule za sekondari na maboma ya madarasa 700 shule za msingi.

Pia Ujenzi wa shule mpya 184 za sekondari, nyumba za walimu 211 ambapo kati ya hizo 184 ni za sekondari na 27 za msingi,Ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwenye shule za sekondari 400.

Pia Mchengerwa amesema,Mwaka 2025/26, Taasisi za Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakadiria kukusanya Kodi ya Majengo, Maduhuli na Mapato ya ndani ya shilingi trilioni 1.92 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.60 iliyoidhinishwa mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la shilingi bilioni 324.83 au asilimia 20.29.

“Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 56.10 ni za taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, shilingi milioni 306.07 ni Maduhuli ya Mikoa na shilingi trilioni 1.68 ni za mapato ya ndani ya halmashauri na shilingi bilioni 188.96 ni Kodi ya Majengo.”

Kwa mujibu wa Mchengerwa Mwaka 2025/26 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuchangia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika sekta ya elimumsingi, sekondari, afya ya msingi, miundombinu ya barabara, majengo ya utawala, kilimo, mifugo, uvuvi, mazingira, ardhi, utawala bora na uwekezaji katika biashara ya kaboni.

Kuhusu masuala ya lishe amesema,katika mwaka 2025/26, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi bilioni 502.09 za ruzuku ya matumizi mengineyo, fedha za maendeleo za serikali kuu na washirika wa maendeleo kutekeleza shughuli mbalimbali.

Amezitaja shughuli hizo kuwa ni kuendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 43,Ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali za halmashauri 142, vituo vya afya 185 na zahanati 185 na kuwezesha upatikanaji wa watumishi 400 wa mkataba watakaofanya kazi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Pia  kuratibu ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya 175 (hospitali 25, vituo vya afya 50 na zahanati 100) na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma ya Afya ya Msingi 175 (Hospitali 25, Vituo vya Afya 50 na Zahanati 100) vitakavyokarabatiwa au kujengwa kupitia Programu ya Uwekezaji katika Afya ya Mama na Mtoto Tanzania.