January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yaonya watoa Rushwa uchaguzi serikali za mitaa

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imevitaka vyama vya siasa kuzingatia kanuni na sheria zinazosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na wagombea wote kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Rai hiyo imetolewa juzi na Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma wa Taasisi hiyo Mkoani hapa, Happiness Madeghe alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Taasisi hiyo Mjini hapa.

Amesema kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika nchini mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu utaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni zitokanazo na Sheria za Serikali za Mitaa na Mamlaka za Miji sura namba 288 na namba 287.

Amefafanua kuwa sheria hizo zinabainisha wazi mambo yasiyoruhusiwa kufanywa na chama cha siasa au mgombea yeyote wakati wa mchakato wa kupata wagombea, kwenye kampeni na wakati wa uchaguzi.

Madeghe ametaja mambo yasiyoruhusiwa kuwa ni pamoja na kutoa rushwa ili kumshawishi mtu yeyote kupiga kura, kugombea au kujitoa katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya uongozi.

Mengine ni kukodi au kutumia usafiri wa aina yoyote kubeba na kusafirisha wapiga kura kwa madhumuni ya kushawishi wapiga kura, kununua kura au kutoa rushwa ya aina yoyote ile au vifaa kwa wapiga kura au msimamizi wa uchaguzi.

Amesisitiza kuwa sheria zinazosimamia uchaguzi na sheria ya TAKUKURU namba 11 ya mwaka 2002 zinatamka bayana kuwa kununua au kuuza kadi ya mpiga kura wakati wa mchakato wa uchaguzi ili kumzuia kupiga kura ni kosa la rushwa.

Makosa mengine ni kutoa rushwa kwa mgombea ili kumshawishi ajitoe, kutoa rushwa ili uteuliwe kugombea, kuomba au kupokea rushwa ili kumteua mgombea na kutoa rushwa ili kushawishi wapiga kura wampigie fulani au wasipige kura.

Naye Afisa Mawasiliano wa Taasisi hiyo Mkoani hapa, Edna Adrian amesema kuwa jukumu la kupambana na vitendo vya rushwa ni la kila mtu hivyo akawataka wanahabari kutumia kalamu zao kufichua vitendo hivyo na viashiria vinginevyo.

Amebainisha baadhi ya viashiria vya rushwa kuwa ni ukiukwaji wa taratibu za kisheria na kiutawala kwa makusudi, uzembe katika kutekeleza majukumu ya kazi ikiwemo kuacha kuchukua hatua stahiki au kuchukua hatua zilizo nje ya uwezo.

Viashiria vingine ni huduma kuchukua muda mrefu sana bila sababu za msingi, kuongeza urasimu kwenye utoaji huduma, lugha zenye kushawishi rushwa mfano; jiongeze, mkono mtupu haulambwi, mwone fulani nje ya ofisi na maji ya kunywa.

Akifafanua zaidi Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Abnery Mganga amesisitiza kuwa wameweka mifumo madhubuti ya ulinzi kwa watoa taarifa za rushwa au viasharia vyake hivyo akaomba jamii kuisaidia taasisi hiyo kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kunaswa wale wote watakaojihusisha vp na vitendo vya rushwa.