Na Moses Ng’wat, Songwe.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe imeokoa zaidi ya Shilingi milioni 31,446,000 fedha za matumizi ya asilimia 10 za mapato ya ndani katika Halmashauri ya Mji Tunduma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 23,2024, kwa lengo la kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Frida Wikesi, amesema ufatiliaji uliofanyika juni mosi hadi 30, 2024 Takukuru ilifanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha.
Wikesi amesema katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Juni Mosi hadi 30, 2024 Takukuru imeweza kukusanya kiasi cha shilingi 31,446,000 kutoka katika makundi maalumu 20 kati ya vikundi 151 vilivyokopeshwa fedha hizo za asilimia 10 za mapato ya ndani kutoka kata zote 15 za Halmashauri ya Mji Tunduma.”Uchunguzi umebaini kuwa kutorejeshwa kwa mikopo hiyo ndani ya muda wa marejesho kumechangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo wakopaji kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya mikopo hiyo” amesema Wikesi.
Aidha, Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Songwe amesema sababu nyingine zilizochangia mikopo hiyo kutorejeshwa kwa wakati ni matumizi mabaya ya mikopo kwa kuwa baadhi yao hutumia fedha hizo kwenye matumizi binafsi nje na dhumuni la mkopo.
“Tumebaini pia baadhi ya wanavikundi kukimbia na fedha za mikopo hali ambayo imesababisha baadhi ya wanavikundi wengine kuwalipia wenzao waliokimbia, mikopo kutolewa kwa makundi yasiyo na vigezo pamoja makundi yasiyo hai” amefafanua zaidi Wikesi.
Pia wamefuatilia utekelezaji wa mradi ya maendeleo 39 yenye thamani ya shilingi milioni 13,412,222,945.09 katika sekta za Elimu, Maji, Afya, Kilimo na Miundombinu.
Amesema katika ufuatiliaji huo, miradi 16 yenye thamani ya shilingi milioni 8,249,687,597 ilibainika kuwa na mapungufu kiufundi ambapo tayari ushauri umetolewa ili wahusila waweze kufanya marekebisho.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini