Na Joyce Kasiki,TimesMajira,Online,Dodoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma imemfikisha katika mahakama ya wilaya ya Bahi Emmanuel Mziwanda (61) na kumfungulia shauri la uhujumu uchumi Namba 1/2021.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mkuu Taasisi hiyo mkoani hapo, Sostenes Kibwengo imesema kuwa mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani jana huku uchunguzi wao umeonyesha kuwa ,mshitakiwa ambaye alikuwa Afisa Afya na Mratibu wa Mradi wa Belgium Fund for Food Security (BFFS) wa Halmashauri ya wilaya ya Bahi,aliandaa nyaraka za kuonyesha matumizi ya shilingi 15 milioni kama gharama za mafunzo kwa maafisa ugani 60.
“Uchunguzi umeonyesha kwamba,mafunzo hayo aliyoyaandaa hayakufanyika na maafisa Ugani hao hawakulipwa posho hizo bali mshitakiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia ya udanganyifu.” Amesema Kibwengo na kuongeza kuwa
“Baada ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuridhika na ushahidi uliokusanywa iliruhusu mtuhumiwa kufikishwa mahakamani ambapo amesomewa mashtaka manne, matatu yakiwa ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume cha sheria ya TAKUKURU na moja la kusababisha hasara ya shilingi 15 milioni kinyune cha sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2002.”
Kibwengo amesema mtuhumiwa amepelekwa rumande kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana kwa mashtaka husika .
Aidha Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani Dodoma amewahimiza watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwani madhara yake ni makubwa na ni kikwazo cha maendeleo ya Taifa.
Mnamo Oktoba 2019 ,TAASISI hiyo ilimkamata Mziwanda kwa tuhuma za kuisababishia hasara Serikali ya shilingi 15 milioni kwa kughushi nyaraka na kumdanganya mwajiri wake.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito