Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MIRADI ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh bil 430 iliyotekelezwa na serikali Mkoani Tabora imefanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kujiridhisha kama thamani ya fedha (value for money) inaendana na kazi iliyofanyika.
Akizungumza na vyombo na habari juzi Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa Mussa Chaulo amesema kuwa jumla ya miradi 18 iliyotekelezwa katika maeneo mbalimbali Mkoani humo kwa gharama ya sh 432, 485,799,821/= imefuatiliwa.
Amebainisha kuwa kati ya miradi hiyo, miradi miwili mmoja wa shule ya msingi Kakola wenye thamani ya sh 603,890,000/= ilibainika kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo wazabuni waliotoa huduma kutolipwa stahiki zao.
Mradi mwingine uliobainika kuwa na kasoro ni wa ujenzi wa nyumba 2 za walimu (two in one) uliotekelezwa kwa fedha za ufadhili wa Taasisi ya Elimu (TEA) kwa gharama ya sh 210,000,000/= katika shule ya sekondari Chetu.
Chaulo amefafanua baadhi ya kasoro zilizobainika kuwa ni kutozingatiwa michoro (ramani) hali iliyopelekea baadhi ya miundombinu kutojengwa inavyotakiwa, ujenzi kuwa chini ya kiwango, baadhi ya kuta kupinda na rangi kutopigwa vizuri.
Amesema kuwa baada ya kubaini kasoro hizo walimwelekeza Msimamizi wa Mradi (Mkuu wa shule) kurekebisha mapungufu yote yaliyopo katika mradi huo, agizo hilo lilitekelezwa kikamilifu.
Kwa upande wa wazabuni waliotoa huduma mbalimbali kutolipwa stahili zao wamemshauri Msimamizi wa Mradi kuhakikisha anawalipa fedha zao kwa wakati kwa kuzingatia taratibu za malipo vinginevyo anaweza kuchukulia hatua zaidi.
Aidha Chaulo amebainisha kuwa pia wamefanya uchunguzi wa mifumo mbalimbali ikiwemo ya ukusanyaji na uondoshwaji taka lengo likiwa kuboreshwa utoaji huduma hizo na kupunguza kero zinazosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Mifumo mingine iliyofanyiwa uchambuzi ili kuboreshwa zaidi ni utoaji huduma za Sekta ya Ardhi katika Ofisi za Halmashauri, Utendaji kazi kwa Watumishi wa Vyuo vya Kati na Utoaji elimu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa umma.
Chaulo ameongeza kuwa Taasisi hiyo pia imefanikiwa kuokoa zaidi ya sh mil 117 ambazo ni fedha za wakulima wa tumbaku wa Chama Cha Msingi Kisanga (Amcos) cha Wilayani Sikonge ambazo hawakulipwa katika msimu uliopita.
Amesema fedha hizo zimeokolewa baada ya taasisi hiyo kufanya uchunguzi dhidi ya wakulima na viongozi wa Amcos hiyo waliofanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha sh bil 3.6 walizokopeshwa na benki ya NMB kwa ajili ya kilimo cha tumbaku kwa msimu wa mwaka 2022/2023.
Amefafanua kuwa baadhi ya Viongozi walitorosha tumbaku na kuuza kusikojulikana hali iliyosababisha baadhi ya wakulima kutolipwa fedha zao wakati wa malipo na chama hakikuwa na fedha.
Amesema kuwa baada ya TAKUKURU kufanya uchunguzi wa kina na kuwabana wahusika wote, baadhi ya viongozi na wakulima wamerejesha jumla ya sh mil 117 na baadhi yao bado wanaendelea kurejesha.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â