Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma,imebaini kuwepo kwa mapungufu katika miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 4,344,553,908.
Hayo yamesemwa jijini hapa jana na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma,Asha Kwariko wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Disemba 2023.
Kwariko ametaja baadhi ya miradi iliyofanyiwa ukaguzi kuwa ni ujenzi wa miundombinu ya maji Kijiji cha Pahi,wilayani Kondoa,ambapo waliabaini uchimbaji wa mtaro haukuzingatia specification.
Mwingine ni mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Manungu ambapo walibaini milango iliyowekwa kwenye choo cha wasichana kuwa chini ya kiwango tofauti na specification na imenunuliwa kwa bei kubwa.
Amesema wao kama TAKUKURU walichukua hatua za kwa kutoa ushauri wa uzingatiaji wa specification na ufuatiliaji ufuatiliaji unaendelea,katika ujenzi wa shule ya sekondari walitoa ushauri kuhusiana na kubadilisha/kurekebisha milango ya choo.
Vilevile amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu walipokea jumla ya malalamiko 165 kati ya hayo malalamiko 90 hayakuhusu rushwa na 75 yalihusu rushwa .
“Kati ya malalamiko 90 ambayo hayakuhusu rushwa malalamiko 72 walalamikaji wake walielimishwa,malalamiko matano yalihamishiwa idara nyingine na malalamiko 13 walalamikaji wake walishauriwa namna bora ya kutatua malalamiko yao,”amesema.
Amesema kuwa kwa malalamiko 75 yaliyohusu rushwa yalipelekea kufunguliwa majalada 19 umekamilika na majalada matano mashauri yake yamefunguliwa mahakamanina majalada 51 uchunguzi wake bado unaendelea.
Pamoja na hayo Kwariko ametaja vipaumbele vya TAKUKURU mkoa wa Dodoma kwa Januari hadi Machi 2024 kuwa ni kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya rushwa na ufujaji unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Hii ni pamoja na kufuatilia miradi ya ujenzi wa madarasa,vituo vya afya na miradi mingine ambayo bado inaendelea kujengwa kupitia fedha za kuimarisha Elimu ya awali na msingi,”amesema.
Amesema kipaumbele kingine ni kufuatilia kero za migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikilalamikiwa kila kukicha.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba