Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.
UZEMBE kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi umetajwa kuwa chanzo cha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Ripoti ya robo ya nne ya mwaka inayoanzia April hadi Juni, 2024 iliyotolewa Julai 30, 2024 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imebainisha hayo.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Atuart Kiondo akiwasilisha ripoti hiyo ofisini kwake kwa waandishi wa habari amesema taasisi hiyo ili kudhibiti uzembe imechukua hatua.
Kiondo ametaja hatua hizo ni kurejesha fedha Mil 150 kati ya Mil 300 fedha ambazo zilikusudiwa kulipwa kwa mzabuni wa utengenezaji wa samani za Ofisi ya Halmashauri ya Mlele kama malipo ya awali kuwa kinyume na makubaliano ya kimkataba kati yake na halmashauri hiyo.
Wakati huo fedha Mil 1.9 zimeokolewa, ambazo zilitakiwa kutengeneza viti na meza za wanafunzi “Samani hizo zilitengenezwa chini ya kiwango na huu ni uzembe wa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mlele” amesema Kiondo.
Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU amebainisha kuwa taasisi hiyo ili kuhakikisha wasimamizi hao wanatoa fedha zao na kuwezesha kutengeneza vitu 30 na meza 30 ambazo ziko kwenye kiwango kinachotakiwa na kukabidhiwa shule ya sekondari Kamalampaka Wilaya ya Mlele.
Kiondo ameongeza “ Tumerejesha zaidi ya fedha Mil 20 za makusanyo ya POS zilizokuwa anadaiwa mkusanya ushuru wa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele za kipindi cha April, 2020 hadi Mei, 2021 na kuzirudisha benki kwa mujibu wa sheria”.
Katika hatua nyingine ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo jumla ya miradi nane yenye thamani ya Bilioni 8.91 katika sekta ya elimu,Uchumi na Biashara na Miundombinu imefuatiliwa na kubaini mapungufu ikiwemo ucheleweshwaji wa miradi,malipo kwa wakandarasi na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.
Vilevile katika kudhibiti uzembe wowote kwa watumishi wa umma,TAKUKURU Mkoa wa Katavi inaendelea kufanya uchambuzi wa mifumo ikiwa na lengo la kubaini mianya ya rushwa na kuidhibiti.
Kiondo ametoa wito kwa watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, hasa wataalamu wa ujenzi wasimamie miradi ya maendeleo kwa umakini na uandilifu, huku wakizingatia thamani ya fedha.
Secilia Chambi, Mkazi wa wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi ameiomba TAKUKURU kuchukua hatua za kuwapeleka mahakamani wale wote wanabainika kujihuisha na uzembe unaopelekea matumizi mabaya ya fedha za umma.
Amesema kuwa usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo unasababisha kuchelewa kwa miradi kukamilika kwa wakati,Kuzorota kwa ubora,Ongezeko la gharama,kupotea kwa rasilimali na kupungua kwa imani ya watu kwa serikali yao.
Samson Zakayo, Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi amesema kuwa TAKUKURU inapaswa kutoa elimu zaidi kwa wananchi kwamba wana nafasi kubwa ya kuisimamia miradi ya maendeleo na endapo ubadhirifu wowote ambao unaweza kujitokeza kwenye miradi hiyo waweze kutoa taarifa haraka kwa taasisi hiyo.
Zakayo ametoa ushauri kwa serikali kuanzisha mtaala maalumu wa elimu kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu wa somo la uzalendo na utaifa utakao weza kuchochea watu kuipenda nchi yao na kudhibiti vitendo vya ubadhirifu na rushwa.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote