Na Jackline Martin, TimesMajira Online
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Temeke imewasimamisha kazi maafisa wawili wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kutokana na uzembe uliopelekea kuchelewesha uanzishwaji wa miradi miwili ya maendeleo inayotekelezwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.
Watumishi hao ni Restituta Mtaita aliyekuwa na Divisheni Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kigamboni, na Joseph Mhere aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi wa Manispaa ya Kigamboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Mkuu wa TAKUKURU (M) Temeke, Ismail Bukuku, alisema ufuatiliaji uliofanyika ni wa miradi yenye thamani ya sh.milioni 700 na ilihusu ujenzi wa shule mpya mbili za sekondari.
Sekondari hizo Vumilia Ukooni iliyotengewa kiasi cha sh. milioni 350 na sekondari Mbutu iliyotengewa kiasi hicho hicho.
“Baada ya kuwasilisha matokeo ya ufuatiliaji wetu kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo watumishi waliohusika na uzembe huo walcihukuliwa hatua za kinidhamu.
Sambamba na kutoa ushauri huo, ofisi itapita tena kwenye miradi hiyo ili kuona namna ushauri huo ulivyotekelezwa,” alisema.
Bukuku aliwataka watumishi wote kutimiza wajibu wao wa kusimamia kwa uadilifu na uaminifu miradi yote kwa kuwa wameaminiwa katika taasisi wanazozihudumia kwa kuwa kutokufanya hivyo ni kinyume na Kif. 31 PCCA.
Pia aliwataka wananchi wote kushiriki kusimamia miradi ya umma na kutoa taarifa mapema TAKUKURU juu ya miradi inayotekelezwa katika maeneo yao pale wanapoona miradi hiyo inadorora au kuna ubadhilifu wa aina yoyote.
Aidha, Bukuku alisema TAKUKURU Temeke kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke walifanikiwa kudhibiti ujenzi wa maghala uliokuwa unafanyika tofauti na kibali cha ujenzi kilichotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.
“Mkurugenzi huyo alitoa kibali cha ujenzi wa ghala 1 eneo la Buza kwa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam -Buza, lakini ujenzi uliokuwa unafanywa na kanisa hilo ni maghala matatu badala ya moja.
Aidha vipimo vya maghala hayo havikulingana na vipimo vilivyotolewa na Mkurugenzi huyo kwa ghala lililopewa kibali, kutokana na hali hiyo, kanisa lilitozwa faini ya sh. 14, 134,439.30.”
Pia Bukuku alisema pamoja na kufanya mikakati na juhudi za kuzuia rushwa na uelimishaji umma, bado wapo wananchi wachache ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema katika kipindi husika, walipokea malalamiko 63 ambapo malalamiko 54 yanahusu rushwa na 9 hayahusu rushwa.
“Malalamiko yaliyohusu rushwa yanafanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha tuhuma na yapo katika hatua mbalimbali na yasiyohusu rushwa walalamikaji walielimishwa na taarifa zikafungwa”
Bukuku alisema katika robo ya Aprili Juni, 2024 wanatarajia kuendelea kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa katika utoaji wa huduma za jamii, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki katika vita dhidi ya rushwa kupitia Programu mbalimbali ikiwemo programu ya TAKUKURU Rafiki.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi