December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Takukuru Mbeya yamshikilia mtalaam wa mionzi hospitali rufaa mkoa wa Mbeya

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

TAASISI ya kuzuia na  kupambana na Rushwa(Takukuru) Mkoa wa Mbeya inaendelea kumshikilia Mtalaam wa mionzi katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya , Labert Haule kwa kudaiwa kujifanya ofisa Takukuru  na kuchukua fedha kwa wananchi kwa madai ya kuwasaidia kesi zao ili waachiwe huru na kufutiwa mashtaka yanayowakabili.

Kwa mujibu wa  Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mbeya ,Maghela Ndimbo amesema hayo leo wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu kutoka  mwezi Januari hadi marchi mwaka huu.

Ndimbo amesema kuwa tayari wamemkata mtalaam huyo ila wanasubiri kibali  toka  kwa mkurugenzi wa mashtaka  mara baada ya uchunguzi kukamilika  na kupata kibali  ili aweze kufikishwa mahakamani .

“Hivi  sasa sheria imebadilika sana mtu yeyote  akikamatwa lazima uchunguzi ukamilike kwanza  tofauti na zamani mtu anakamatwa anapelekwa mahakamani huku uchunguzi ukiendelea kufanyika hivi sasa haipo hivyo”amesema Mkuu huyo wa Takukuru .

Hata hivyo Mkuu huyo Takukuru amesema  kwamba mara  nyingi  watu wanaojifanya maafisa Takukuru wamekuwa wakitumia simu ambazo wamesajili kwa majina yasiyo yao kufanya matukio hayo ya udanganyifu kwa wananchi na pale wananchi wanapohitaji kuonana nao huwa hawakubali  na kudai fedha watumiwe kwa njia ya simu  ambazo wamesajili kwa majina ambao siyo yao .

Aidha Ndimbo ametoa onyo kwa watu wanaojifanya maafisa Takukuru kwa kuwalaghai wananchi  kuwa wana uwezo wa kuwasaidia kutokana na na kutuhumiwa kwa makosa mbali mbali  ili waachiwe na kufuta mashtaka  ya uongo wanayodai  yanayowakabili  baadhi ya wananchi .

Akielezea zaidi Ndimbo amesema kuwa watu hao wanaojifanya maafisa wa Takukuru wamekuwa wakiwasingizia wananchi  kadhaa kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya Rushwa TAKUKURU  wakati sio kweli  na hatimaye kuwaomba fedha ili wawasaidie haja yao ni kuwatapeli kwani hawawezi kulifanya.

“Takukuru ipo kazini inaendelea na uchunguzi wa kuwatafuta  watu hao watakamatwa  na hatimaye kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu  wa sheria , tumebaini kuwa vitendo hivi vimekuwa vingi lazima watu hawa tuwakamate”amesema Ndimbo.

Aidha Mkuu huyo wa Takukuru amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu waliweza kufanya uchunguzi sekta ya elimu  kwa upande wa walimu kujihusisha na rushwa ya ngono na wasimamizi wa sekta ambapo walibaini  mapungufu  kadhaa  ikiwemo ukosefu wa maadili  kwa baadhi ya watumishi  wa sekta ya delimu kujirahisi kwa walimu wa kike ili waweze kupangiwa shule zilizoko mjini  na kutaka madaraka bila kufuata utaratibu.

Ndimbo amesema kuwa baada ya kubaini mapungufu hayo walikaa vikao na wadau  wa sekta ya elimu  kwa ajili ya kuondoa mianya ya rushwa  iliyobainika na kuwekeana mikakati ya ufuatiliaji .

Amesema  kuwa tayari wamefanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo (26) yenye thamani ya Bil.18 ambapo miradi hiyo ni Afya, Elimu,Maji,Barabara na madini ambayo ilikuwa na changamoto ya utekelezaji.

“Kati ya miradi hiyo baadhi tulikuta ina kasaro kubwa zilizosababisha uchunguzi kuanzishwa ni mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Mbarali  ambapo awamu ya kwanza ulikuwa na thamani ya zaidi ya Bl.2.500”amesema .

Alisema  baada ya ufuatiliji wa kina  mradi huo ulikutwa na kasoro kadhaa ikiwemo kujengwa chini ya kiwango na hivyo kuifanya Takukuru  mkoa wa Mbeya kuanzisha uchunguzi wamatumizi halisi ya fedha zilizotumika kutekeleza mradi huo.

Amesema  kuwa mradi mwingine uliofutiliwa ni ujenzi wa Mzani wa barabara ya Makongorosi Chunya  wenye  thamani  ya shilingi 7,539 Bilioni  na kulazimika kuanzisha uchunguzi baada ya  kubaini  kutengwa  kiasi kikubwa cha fedha kuliko uhalisia.
 
“ Tumebaini kuwepo kwa changamoto ya  malalamiko kutoka kwa wananchi ya uwepo wa malipo hewa ya fidia kwa   waliopisha maeneo yao ili  kupisha mradi huo uweze kujengwa  hivyo Takukuru tayari imeanzisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

Akizungumzia kuhusu watu wanaojifanya maafisa Takukuru ,Mkazi wa Sai  Jijini Mbeya Faraja Juma amesema kuwa suala la maafisa vishoka limekuwa kero katika maeneo mbali mbali hasa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni .

“Tunashukuru Takukuru wameliona hili tunaomba watusaidie tunaliwa sana hela na hawa watu na wanachukua fedha nyingi kwa madai ya kutusaidia “amesema faraja.