November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Manyara yamshikilia Mwendesha Mashtaka kwa rushwa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Babati

MWENDESHA mashtaka wa Mkoa wa Manyara,Mutalemwa Kishenyi anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni tano.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo Mjini Babati wakati akizungumza Aprili 25, mwaka huu.

Makungu amesema kwamba Mwendesha mashtaka huyo wa Mkoa wa Manyara, wakili Kishenyi amekamatwa Aprili 23 mjini Babati usiku akiwa anapokea kiasi cha shilingi milioni tano kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika upekuzi uliofanywa na mamlaka za dola ambapo walikamatwa na risasi 370 na stika bandia zenye thamani ya shilingi bilioni sita.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema kuwa Mwendesha mashtaka huyo alikamatwa wakati akipokea rushwa ili kuwasaidia watuhumiwa hao.

“Uchunguzi zaidi wa tuhuma hizi unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa huyu atafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma husika,” amesema Makungu.