Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara huku miundombinu hiyo ikikabiliwa na hatari kubwa ya kuharibika kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Ambapo takribani bilioni 209.7, zilitumika kufanya matengenezo ya dharura kati ya mwaka 2015 na 2020.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Ujenzi Godfrey Kasekenya wakati akifungua warsha ya siku mbili ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia chi mwenye miundombinu ya barabara na uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara,iliyofanyika jijini Mwanza ambayo kauli mbiu yake ni “Athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara; mikakati na mbinu za kukabiliana nayo”.
Kasekenya ameeleza kuwa kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi,serikali iliandaa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kunzia 2021 hadi 2026 (National Climate Change Response Strategy 2021-2026).
Ambapo ameeleza malengo yake ni pamoja na kujumuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwenye mipango na bajeti za kisekta na kuwezesha upatikanaji endelevu wa fedha na teknolojia ili kukabiliana na madhara hayo.
“Napenda kuipongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kuandaa warsha ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko tabianchi kwenye miundombinu ya barabara,matumaini yangu kuwa matokeo ya warsha hii yatasaidia katika kuandaa mpango kabambe wa kisekta wa kutekeleza mbinu mbalimbali ambazo zitasaidia kuilinda rasilimali hii muhimu kwa taifa,”ameeleza Kasekenya.
Pia ameeleza kupitia warsha hiyo ametoa changamoto kwa washiriki kudhamiria kufanya tafiti mahsusi ili kuona jinsi bora ya kutekeleza kazi za barabara na utunzaji wa miundombinu yake.
“Ni muhimu sasa kuhakikisha kwamba, tunatenga fedha kila mwaka ili kugharamia shughuli za utafiti ambao utajikita zaidi katika kuleta teknolojia ya ujenzi au matengenezo ya barabara ambayo itastahimili athari za mabadiliko ya tabianchi pia ulenge katika kuongeza matumizi ya malighafi inayopatikana hapa nchini, hususani kwenye maeneo ya mradi kama vile mawe na vifusi na changarawe,”ameeleza Kasekenya.
Aidha ameeleza kuwa ili kukabiliana na upungufu wa fedha za matengenezo ya barabara serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya mapato ya mfuko wa barabara kila inapowezekana huku Halmashauri zikitakiwa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kugharamia matengenezo kwenye maeneo yao.
“Ni wajibu wa viongozi wa Serikali za Mitaa kusimamia ulinzi wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo yao,kupitia viongozi hawa, athari zinazotokana na wizi wa samani za barabara, matengenezo ya magari barabarani na mifugo kutembea barabarani zitapungua na mwisho kutoweka kabisa,”ameleeza.
Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Barabara Eliud Nyauhenga, ameeleza kuwa ili kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa hali ya barabara,bodi iliamua kuunda mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji (e-Monitoring) ili kutoa taarifa kuhusu hali ya barabara ambapo mfumo huu unalenga kuwashirikisha wananchi hasa watumiaji wa barabara katika kusimamia na kutunza miundombinu ya barabara.
Kupitia mfumo huo taarifa za hali ya barabara kutoka kwa watumiaji wa barabara zitapelekwa kwa meneja wa TANROADS na TARURA pamoja na Bodi ya Mfuko wa Barabara ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kupeleka mrejesho kwa watoa taarifa.
“Mfumo huu umeshafanyiwa majaribio sehemu mbalimbali kwa kutumia makundi mbalimbali ya wadau na kuonesha matokeo mazuri,wananchi wanaweza kutumia simu-janja (smart phones) au simu za kawaida (kitochi au kishikwambi au kiswaswadu) kutuma taarifa kwa kutumia mfumo huu ni pamoja na mashimo hatarishi, ujenzi mbovu, kuziba mifereji, kuibiwa alama za barabarani na kadhalika,”ameeleza Nyauhenga.
Pia ameeleza kuwa ni sera ya bodi hiyo kuhamasisha watendaji kuwa wabunifu wakati wa kutekeleza kazi za barabara hasa kwa kutumia malighafi inayopatikana sehemu ya mradi.
“Ubunifu wa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye maeneo ya mradi hupunguza gharama za ujenzi na hivyo kuokoa fedha za serikali vilevile huongeza ajira kwa wakina mama na vijana na hivyo kusaidia kupunguza umaskini,”.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best