December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taharuki yazuka jeneza lakutwa mlangoni kwa mwalimu mkuu

Na Steven Augustino,TimesMajira Online,Namtumbo

DIWANI wa kata ya Likuyu wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma Kassimu Gunda amekasirishwa na kitendo kilichofanywa na watu wasiojulikana kwa kuweka jeneza usiku wa manane nyumbani kwa mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mfuate.

Diwani Gunda ambaye alidai kupata taarifa hiyo kwa njia ya simu Februari 23, mwaka huu, alfajiri alilazimika kwenda nyumbani kwa mwalimu huyo na kulikuta jeneza hilo ambalo huwa linahifadhiwa msikitini likiwa limewekwa mbele ya mlango wa nyumba ya mwalimu huyo.

Kufuatia hali hiyo Diwani Gunda aliamuru jeneza hilo liondolewe na kurudishwa msikitini na kuitisha kikao cha wazee wa kijiji hicho pamoja na kamati ya shule kujadili kitendo cha baadhi ya wananchi kumwekea jeneza mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mfuate na kuibua taharuki kwa walimu.

“Walimu hawa ndio wanaonisaidia mimi diwani kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha wanafunzi kutoka awali mpaka darasa la saba wa shule ya Mfuate wanapata elimu,na ili walimu hao wafundishe vizuri na kutekeleza ilani ya chama wanahitaji kupata utulivu katika kazi ya kufundisha “alisisitiza diwani huyo.

Kwa mujibu wa diwani zoezi la kuwapata waliofanya kitendo hicho wamepewa wazee wawili wa kijiji hicho ambao hakuwataja majina yao na mara watakapopatikana hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kudhibiti tabia za ovyo wanazofanyiwa walimu.

Akizungumzia kadhia haiyo mwalimu mkuu wa shule hiyo Peter Haule kwa upande wake pamoja na mambo mengine alimshukuru diwani wa kata hiyo namna alivyompa ujasiri wa kuliona tukio hilo kama ni changamoto katika maisha lakini kabla ya kuja diwani huyo alisema akili yake haikuwa vizuri hasa akilitazama lile jeneza na alitamani kufunga mizigo yake na kwenda ofisi ya mkurugenzi .