Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline.Dar
CHAMA cha Wakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) kimepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za upakiaji na upakuzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kuwataka wanaobeza jitihada hizo kupuuzwa.
Akiongea katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TAFFA, Edward Urio, alisema kuwa bandari ya Dar es Salaam kupitia uwekezaji uliofanywa na ushirikishwaji wa sekta binafsi imekuwa na mafanikio makubwa ya kujivunia katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita.
“Tukiwa kama wadau wakubwa wa usafirishaji na upakuaji wa mizigo Bandarini, tunajivunia sana uwekezaji mkubwa uliofanyika na tunakwazika na watu wanaopinga maendeleo hayo kwa namna moja au nyingine,”alisema Urio.
Alisema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha ufanisi unaongezeka katika utoaji huduma katika Bandari ya Dar es Salaam ili kuvutia zaidi wawekezaji, bado kuna watu kupitia mitandao ya kijamii wanapotosha jamii na kurudisha nyuma jitihada hizo.
“Upotoshaji huu unaharibu sifa ya bandari yetu ambayo inategemewa na zaidi ya nchi nane katika kupitisha mizigo yao na itaweza kuchangia kupungua kwa mizigo na mapato kupungua,” alisema.
Alisema kuwa katika siku za hivi karibuni, Taffa imeona video mbalimbali zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinazotoa taarifa ambazo ni za upotoshaji kwa umma wa Watanzania.
“Tukiwa kama wadau tunaowakilisha zaidi ya wanachama 1483 wanaofanya kazi za kuondoa shehena sehemu mbalimbali ikiwemo bandarini na viwanja vya ndege, tunafurahia mapinduzi makubwa yanaoyoendelea katika bandari yetu,”
“Ukitofautisha na miaka mitatu iliyopita, ufanisi katika bandari yetu umeongezeka baada ya uwekezaji mkubwa kufanyika,” alisema.
Alisema uwekezaji huo uliogharimu takriban dola milioni 600 katika upanuzi wa utoaji huduma kuanzia gati namba 0-7 na upanuzi wa kina cha maji na eneo la kugeuzia meli.
Hatua hii amesema imesaidia kupunguza muda wa meli kupakua mizigo kutoka wastani wa siku 25-30 zilizokuwa zinatumika hapo awali kabla ya uwekezaji wa DP World hadi kufikia wastani wa siku 3-5 kwa sasa.
Alielezea faida ya hatua hii kuwa imepunguza gharama ambapo wastani wa gharama kwa meli moja kupaki nje ya geti kwa siku ni kuanzia dola 10,000 ( takriban milioni 25) na mwisho wa siku gharama hizi moja kwa moja zilimuathiri mtu wa mwishoa ambaye ni mwananchi wa kawaida.
Kwa mujibu wa Urio, maboresho haya yamepelekea kuvutia wateja wengi kutumia bandari ya Dar es Salaam kupitia jitihada mbalimbali zinazoendelea, ikiwemo usafirishaji wa mizigo hiyo kwenda sehemu mbalimbali, ikiwemo bandari kavu zilizopo ndani na nje ya nchi kwa njia ya reli.
Pia amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza kasi ya kutoa huduma kwa kupitia mfumo mmoja bandari hapo ili kuhakikisha shehena za mizigo zinahudumiwa kwa haraka pindi zinapowasili bandarini hapo.
Kupitia maboresho haya, amesema Taffa inajivunia kuwa sehemu ya makusanyo makubwa ya kodi yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kupitia bandari.
“Kamishina wa TRA alishafanya kikao na Taffa na kupongeza mchango wetu kama sekta binafsi katika kutoa huduma bora yenze ushindani miongoni mwetu ili kuvutua wateja zaidi,” alisema Urio.
Katika kuhakikisha mafanikio na changamoto zinazohusu bandari zinajadiliwa na kutatuliwa, Urio amesema kumekuwa na kikao kinachofanyika kila mwezi ( Port Import Council) ambao wadau hukutana.
kwa kupitia jitihada mbalimbali katik ya serikali na sekta binafsi, mafanikio mbalimbali ya kiutendaji yanayoonekana na ni miongoni mwa mafanikio ambayo taasisi yake inajivunia.
Alisema mafanikio haya yametokana na Serikali kutambua mchango wa sekta binafsi na kuzidisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja