Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Dodoma
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuwanufaisha Watanzania baada ya kutoa mkopo wa sh. 1,101,687,500 kwa Vijana wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwa ajili ya kujishughulisha na shughuli za ufugaji.
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ndiyo alikabidhi mfano wa hundi kwa vijana hao kwenye kilele cha Maonesho ya Nanenane ya Kimataifa yaliyofanyika kwa mara ya kwanza Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma.
“Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa kiasi cha sh. 1,101,687,500 kwa vikundi 25 vya vijana wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) walio chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao wamehitimu mafunzo ya ufugaji wa kibiashara kupitia programu ya unenepeshaji mifugo.
“Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na TADB, imeandaa utaratibu wa kuwakopesha vijana mikopo isiyo na riba na yenye masharti nafuu,mikopo hii ni ya muda wa miaka miwili na itaanza kurejeshwa baada ya miezi tisa, wakati kijana atakuwa ameshafanya biashara kwa mizunguko mitatu,Baada ya kumaliza marejesho, kijana atakuwa na fursa ya kuomba tena,lengo ni kufanya mikopo hii iwe inazunguka na kuwanufaisha vijana wengi zaidi”kwamujibu wa taarifa ya benki hiyo.
Akikabidhi hundi hiyo, Rais Dkt. Samia amewasihi vijana hao kutumia kiasi hicho cha pesa ili kujiletea maendeleo na pia wawe mfano wa kuigwa na makundi mengine ya vijana nchini Tanzania.
“Serikali imejitolea kuwekeza kwenu ninyi vijana, kwani ndio nguvu kazi ya taifa, nchi inawatazamia kufanya mabadiliko makubwa kwenye uchumi wa nchi yetu” alisema Rais Dkt Samia.
Taarifa hiyo iliongeza, mnamo Juni 30, 2024, jumla ya vijana 158 walihitimu mafunzo ya Program ya BBT ya ujuzi katika unenepeshaji kutoka katika vituo vinane (8) ambavyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilikuwa ikivisimamia kupitia taasisi za TALIRI vituo viwili na LITA vituo sita.
“Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliandaa utaratibu wa kuwaandalia vitalu vijana hao katika Ranchi za Taifa za Kagoma na Kitengule wilayani Karagwe. Lengo la mkopo huu usio na riba, ni kutaka vijana waanze uzalishaji kibiashara hasa katika unenepeshaji mifugo kama walivyopata mafunzo” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema, katika bajeti ya mwaka 2022/2023, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi za Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) ilianzisha Programu ya BBT kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana na wanawake kufuga kibiashara kupitia mradi wa unenepeshaji mifugo. wizara ilianza kutekeleza Programu ya BBT kupitia Vituo Atamizi vinane (8) katika mikoa ya Tanga – Buhuri (vituo vitatu), Mwanza – Mabuki (vituo vitatu) na Kagera – Kikulula (vituo viwili).
Ilisema, TADB imekua mdau mkubwa katika kuchangia vifaa muhimu na kuwajengea uwezo vijana wa BBT pamoja na mikopo isiyokua na riba, hiyo ikiwa na lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwawezesha vijana kujiajiri kwenye mifugo kwa maendeleo ya kijana mmoja mmoja na uchumi wa nchi kwa ujumla.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best