January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tabora yaweka mikakati kukomesha ukatili wa kijinsia

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI, Taasisi na wadau wa maendeleo Mkoani Tabora wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimeendelea kuongezea Mkoani humo.

Akizindua kampeni hiyo juzi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Balozi Dkt Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia havikubaliki kwa kuwa vinadhalilisha utu wa akinamama na watoto.

Alisema siku 16 zilizotengwa na serikali kukabiliana na vitendo hivyo watazitumia ipasavyo kwa kutoa elimu kwa makundi yote ya kijamii ikiwemo wanafunzi ili watambue madhara ya vitendo hivyo na kuchukua hatua ikiwemo kutoa taarifa.

Alibainisha kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tayari imelekeza Wakurugenzi wa halmashauri zote, Wakuu wa taasisi za umma na wadau mbalimbali kujiwekea utaratibu wa kufikisha elimu hiyo kwa makundi yote ya kijamii katika maeneo yao.

Mtondoo alifafanua kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio hayo ambayo sasa yamefikia 972 kwa mwaka huu pekee katika Mkoa huo, ambapo matukio 362 wahusika wamefikishwa mahakamani.

Aliitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo ili kupunguza matukio hayo ambapo alibainisha kuwa matukio ya ukatili wa kimwili kwa mwaka huu pekee yalifikia 364 huku ya ubakaji yakiwa ni 23.

‘Tumedhamiria kukomesha ukatili wa aina yoyote ile kwa akina mama, watoto na akina baba, Tabora bila ukatili wa kijinsia inawezekana, naomba wana Tabora wote tusimame imara kupinga ukatili huu’, alisema.

Alitaja baadhi ya madhara yanayosababishwa na vitendo vya ukatili miongoni mwa jamii kuwa ni ulemavu, vifo, tatizo la afya ya akili, umaskini, udumavu na ongezeko la watoto wa mitaani.Aidha Mtondoo alitoa wito kwa wanaume waliofanyiwa au watakaofanyiwa vitendo vya ukatili nao kutosita kutoa taarifa ili wanaowafanyia vitendo hivyo nao wachukuliwe hatua za kisheria kama watu wengine.

Awali Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa huo Panin Kerika alieleza kuwa kampeni hiyo itafanyika kimkakati ili kuhakikisha makundi yote ya kijamii yanafikiwa katika vijiji, kata, tarafa na wilaya nzima.

Alibainisha kuwa kilele cha kampeni hiyo kitakuwa Desemba 10 mwaka huu siku ya Jumamosi ambapo shughuli hiyo itafanyika Kimkoa Wilayani Kaliua, hivyo akatoa wito kwa jamii na wadau wote kuhudhuria siku hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Igunga Mkoani Tabora Sauda Mtondoo akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka halmashauri zote 8 za Mkoa huo baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Picha na Allan Vicent.