November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi za serikali na binafsi zatakiwa kutangaza kazi zao

Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline, Zanzibar

TAASISI za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Binafsi zimetakiwa kuendelea kufanya maonesha ili kutangaza kazi zao pamoja na kukuza uchumi wa nchi, kuleta maendeleo, sambamba na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Makamo wa Pili wa Rais Mstaafu Balozi Seif Ali Iddi huko Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge, Unguja mara baada ya kuyapokea maonesho yaliyopita kwa njia ya kutumia magari ikiwa ni shamrashamra katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema iwapo maonesho hayo yataendelezwa na kudumishwa yatasaidia taasisi hizo kutangaza kazi zao pamoja na kukuza uchumi wa nchi, kuleta maendeleo, sambamba na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na hatimae pato la taifa kuongezeka.

Hivyo Balozi Seif ameitaka Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kuendelea kusimamia maonesho ya kazi zinazofanywa na taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi ili kutoa fursa kwa wananchi kuweza kutambua kazi hizo.

“Maonesho hayo yaendelezwe kwani kupia maonesho wananchi wanapata fursa kufahamu bidhaa au huduma zinazofanywa na sekta husika, hivyo naiomba Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kuendelea kufanya maonesha hayo” amesema balozi Seif.

Naye Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amefahamisha kwamba lengo la maonesho hayo ni kuwapa mwamko wananchi kujituma ili iwe chachu ya kujenga Taifa na kuakisi malengo ya waasisi wa Mapinduzi.

Amesema katika kujenga msingi wa heshima na utu wa mwanadamu ipo haja ya kufanya kazi kwa pamoja na kujenga ushirikiano mkubwa katika kubadilishana uzoefu kati ya taasisi mbali mbali zilizoshiriki maonesho hayo kwani itasaidia kuleta umoja wa Wazanzibar katika kujikomboa na umasikini.

Hivyo Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji imeona ipo haja ya kushajihisha Taasisi hizo kujitangaza kupitia maonesho hayo ili wananchi waweze kufahamu namna ya kupata huduma zinazotolewa na Taasisi mbali mbali nchini.

Kwa upande wa washiriki wa maonesho hayo akizungumza kwa niaba bi Amina Said Ali amesema kuwa amefarajika na hatua hiyo, hivyo hana budi kuishukuru na kuipongeza Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa kuanda maonesho hayo kwani wameweza kujitangaza na kuuza bidhaa zao. Hivyo ameiomba Wizara hiyo kuendeleza maonesho hayo.

Maonesho hayo ya huduma na bidhaa yameshirikisha zaidi ya taasisi 50 za Umma na Binafsi ambapo yalianzia eneo la Amani kupitia Mikunguni, Kinazini, Malindi, Darajani, Michenzani na kupokelewa na Makamo wa Pili wa Rais Mstaafu Balozi Seif katika Mnara wa kumbukumbu ya Mapinduzi Kisonge hatimae kumalizikia katika viwanja vya Maisara mjini Unguja.