December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwa kwenye Viwanja vya Maonesho ya Nane Nane vya Nyakabindi mjini Bariadi, mkoani Simiyu.

Taasisi za fedha zahimizwa kuongeza utoaji mikopo kwa wakulima nchini

Na Bahati Sonda, Simiyu.

TAASISI kifedha hapa nchini zimetakiwa kuongeza mikopo kwa wakulima lengo likiwa ni kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wenye tija, hivyo kusaidia kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.

Agizo hilo limetolewa leo makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi, mkoani Simiyu.

Amesema katika kipindi kilichopita taasisi hizo zilitoa mkopo kwa wakulima kwa asilimia 9, hali inayopelekea kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa mkopo kwa wakulima hao.

Aidha Samia aliwaelekeza watafiti wote hapa nchini wanaofanya utafiti hasa za mbegu bora kutoa tafiti kwa maofisa ugani ili waweze kuzifikisha kwa wakulima, kwani wamekuwa wakifanya tafiti nyingi ambazo haziwafikii walengwa ambao ni wakulima.

Ameliongeza kuwa sekta ya kilimo ni mhimili mkubwa wa pato la Taifa na kwamba imeongezeka kutoka sh. trilioni 25.2 mwaka 2015 hadi sh. trilioni 29.5 mwaka jana.

” Niwatake watafiti wote hapa nchini kutoa majibu ya tafiti zao wanazozipata hususan kwenye suala la mbegu bora kuziwasilisha kwa maofisa ugani ili waweze kuwafikishia wakulima, kwani wamekuwa wakifanya tafiti kutoa lakini hawatoi majibu ya tafiti kwa kwa maofisa hao,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga amesema wizara hiyo imejipanga kurahisisha upatikanaji wa malighafi kwenye viwanda vya ndani, kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, viuadudu sambamba na mbolea kwa bei nafuu.

Awali akizungumza akiwa jengo la Wizara ya Kilimo lililozinduliwa mapema na Makamu wa Rais, Waziri Hasunga amesema jengo hilo litatumika kwa shughuli za utoaji elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa mwaka mzima lengo likiwa ni kuwawezesha kuongeza tija kwenye eneo la uzalishaji.

Waziri huyo aliahidi kuwa jengo hilo na majengo mengine ya kilimo yatumika kuelimisha wananchi juu ya elimu ya lishe kwa lengo la kukabiliana na udumavu wa akili kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambapo imeelezwa kuwa jumla ya watoto milioni 3 hapa nchini wana udumavu wa akili huku mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula ikitajwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye tatizo hilo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ametoa rai kwa Wizara za Kilimo, mifugo na uvuvi kuona umuhimu wa kuwa na kituo maalumu na mahiri ambacho wananchi watakuwa wanajifunza na kupata teknolojia mbalimbali hususan kwenye sekta hiyo kuliko na kituo cha kuhama hama mara kwa mara.

Mtaka ameongeza kuwa ni vyema Wizara ya Kilimo ikaona namna ya kuwa na shughuli itakayoleta tija kwenye jeno hilo. Jengo la Wizara hiyo
lililopo kwenye viwanja vya maonesho ya Nane Nane Nyakabindi mjini Bariadi liligharimu sh. milioni 400.

“Ni vyema Wizara za Kilimo, mifugo na uvuvi zikaona haja ya kuwa na kituo maalumu na mahiri ambacho wananchi watakuwa wanajifunza teknolojia mbalimbali ambazo zitaleta tija kwao badala ya kuwa na vituo vingi vya kuhama hama mara kwa mara,”amesema Mtaka