Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezindua taarifa za utendaji katika Sekta ndogo ya Umeme, Gesi Asilia na Mafuta kwa mwaka 2022/2023 huku akitoa maelekezo  kwa Wizara na Taasisi zinazohusika na sekta ya Nishati kuhakikisha wanasoma taarifa hizo na kuzifanyia kazi ili mafanikio yaliyopatikana katika delta hiyo yalete mabadiliko kwenye maisha ya watu.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa taarifa hizo jijini Dodoma,Dkt.Biteko amesema ,kama mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Nishati hayataleta mabadiliko katika maisha ya watu hayatakuwa na maana.
“Mafanikio lazima yaje na hali halisi ya mabadiliko katika maisha ya watu ,tunataka rasilimali zetu zibadilishe maisha ya watu ,
“Mungu ametupa rasilimali nyingi ambazo kama tukiondoka urasimu tutapata maendeleo makubwa sana.”amesema Dkt.Biteko
Maagizo yaliyotolewa ni kwa Wizara ya Nishati na taasisi zake pamoja na Wizara ya Mipango na uwekezaji kuhakikisha wanatatua changamoto zilizoainishwa katika taarifa hizo na kuzipatia majibu ndani ya kipindi cha miezi mitatu na kutaka kila aina ya fursa iliyoonekana kwenye taarifa hizo ichukuliwe kwa uzito mkubwa na itambuliwe kwamba nani ana uwezo wa kuitumia fursa hiyo ndani ya Serikali na katika taasisi binafsi.
Pia Dkt.Biteko ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha tathmini ya mwaka ujao inahusisha utendaji wa Nishati Safi ya kupikia ili kuweza kujipima kwa usahihi kuhusu utekelezaji wa ajenda hiyo inayopewa kipaumbele na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Vile vile ameagiza kuwekewa kwa mabunio ya suluhisho la matishio yote ya Sekta ya Nishati yaliyoainishwa katika taarifa kati ya mwaka 2023 hadi 2025 ili katika ripoti ijayo changamoto husika zisiwepo ikiwemo suala la kuongezeka kwa mahitaji ya umeme kila mwaka.
Dkt. Biteko pia ameitaka EWURA kupima uhusiano wa rasilimali zilizopo na mafanikio ya watu ambapo amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta lazima yaendane na mabadiliko ya maisha ya watu.
Aidha ameagiza mifumo ya uagizaji mafuta iendelee kuboreshwa baada ya kufanyika utafiti wa kina na kueleza kwamba miundombinu ya mafuta bado inahitajika huku akisisitiza kuwa urasimu usiwepo kwenye Sekta ya Nishati.
Ametumia nafasi hiyo kuipongeza EWURA kwa tathmini ambayo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika ambapo ametolea mfano kutolewa kwa leseni ya kuchimba gesi asilia katika kisima cha Ntorya kilichopo mkoani Mtwara kitakachotoa gesi futi za ujazo milioni 140 kwa siku ambapo leseni ya mwisho ya kuchimba gesi ilitolewa mwaka 2006.
Aidha amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha sekta ndogo ya umeme ambapo amezungumzia mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) kwamba umeshaingiza mtambo wa pili katika gridi ya Taifa kupitia mtambo namba 8 na hivyo kufanya mradi huo kuingiza megawati 470 katika gridi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiimarisha Sekta ya Nishati na kusema kuwa Dodoma imeshuhudia matunda ya uimarishaji huo wa sekta kwani sasa umeme haukatiki.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa katika tathmini iliyozinduliwa inaonesha Sekta ya Nishati imepiga hatua kwenye maeneo megi ikiwemo uhakika wa upatikanaji umeme, upatikanaji na usambazaji wa mafuta kuimarika hasa baada ya Mhe. Dkt. Doto Biteko kuanza kuongoza Wizara ya Nishati, aidha upatikanaji na uwekezaji wa gesi unaendelea kuimarika na hii ikijumuisha usambazaji gesi kwenye maeneo mbalimbali kama katika magari, majumbani na viwandani.
Ameongeza kuwa, taarifa ya Benki ya Dunia kwa nchi za Dunia ya Tatu zinazofadhiliwa na Benki hiyo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati kwa Tanzania inafanya vizuri zaidi katika nchi zote zinazoendelea na Bara la Afrika kwa ujumla na hii ni matunda ya usimamizi madhubuti wa Mhe.Dkt. Doto Biteko ambapo eneo lililofanya vizuri zaidi ni usambazaji umeme vijijini na miradi mingine ya nishati kama JNHPP na mradi wa TAZA.
Ameongeza kuwa Benki ya Dunia imeidhinisha Dola.za Marekani milioni 300 ili ziendeleze sekta ya umeme kutokana na ufanisi huo wa Tanzania.
Akitoa taarifa za utendaji katika Sekta ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu ya mafuta, uwekezaji wa vituo vya mafuta na maghala umeongezeka, kuna ongezeko la uagizaji wa Gesi ya Mitungi (LPG) kwa asilimia 16 na ongezeko la uagizaji wa mafuta kwa asilimia 8.
Amesema kuwa katika Sekta ya umeme uwekezaji umeongezeka katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, upotevu wa umeme unazidi kupungua na wateja wa umeme wameongezeka kutoka milioni 3.8 mwaka 2021/22 hadi milioni 4.4 mwaka 2022/2023.
Baadhi ya changamoto zilizoainishwa kwenye taarifa katika sekta ya umeme ni uchakavu wa miundombinu ambao unaendelea kufanyiwa kazi na uwekezaji endelevu kwenye sekta.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto