January 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAA yatakiwa kulipia mirabaha inayohusiana na matumizi ya muziki katika viwanja vya ndege nchini

Na Penina Malundo,Timesmajira

SERIKALI imeitaka  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) kuhakikisha kuwa inazingatia masharti ya kulipia mirabaha inayohusiana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege.

Huku ikitakiwa    kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya nyimbo zinazopigwa ni za Tanzania na asilimia 20 ndio za nje ya Tanzania.

Hatua hiyo imekuja leo baada ya ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA)kusaini  makubaliano ya ushirikiano (MOU) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) ya kulipia mirabaha kutokana na Matumizi ya kazi za Muziki  wa wasanii wa Kitanzania

Akizungumza leo jijini DaresSalaam katika hafla hiyo ,Naibu Waziri  wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amesema makubaliano hayo yaliyoingiwa baina ya Taasisi hizo mbili yatasaidia kuhakikisha kuwa wasanii wa muziki wanapata haki yao ya malipo kutokana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini.

Amesema ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa wasanii wanapata masoko ya kazi zao na kupata mapato kutokana na vyanzo mbalimbali vya kazi zao, na kwamba haki zao zinaheshimiwa kikamilifu.

“Hatua hii ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuhimiza maendeleo ya sekta ya sanaa na muziki nchini,”amesema.

Kwa upande wake Naibu  Waziri wa Uchukuzi,David Kihenzile amesema  ni hatua kubwa  katika kuhakikisha kuwa wasanii wanapata masoko ya kazi zao na kupata mapato kutokana na vyanzo mbalimbali vya kazi zao.

Kihenzile amesema wajibu uliobaki kwao ni kuona kuwa  wasanii wanaendelea kuzalisha kazi zao kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa huku wakizingatia aina na ukubwa wa doko au platform watakayopata kupitia viwanja vya Ndege nchini.

“Natoa pongezi kwa Cosota na Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo  kwa kubuni na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa agizo hilo la  Rais  Samia hivyo natoa wito kwa  taasisi zetu zote za Wizara ya Uchukuzi ikiwemo  ikiwemo TRC,TPA ,LATRA na TASHICO kuwasiliana na COSOTA  na kuiga mfano mzuri iliowekwa na TAA.

Makubaliano hayo yalisainiwa na  Afisa Mtendaji Mkuu  na Msimamizi wa Hakimiliki  COSOTA,Doreeb Sinare na  Mkurugenzi Mkuu wa TAA,Abdul Mombokaleo wakishuhudiwa na Manaibu waziri wa Wizara hizo mbili ambazo zipo chini yao.