May 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Suluhu mgawanyo wa mapato wa huduma za usafiri wa anga nchini, wapatikana

Na Mwandishi wetu, Timesmajira


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) wafanikisha upatikanaji wa suluhu ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na huduma za usafiri wa anga nchini.

Suluhu hiyo imepatikana kupitia kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya pamoja baina ya wakuu wa taasis hizo katika ukumbi wa mikutano wa TAA uliopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tarehe 23 Mei 2025.

Mkataba huo unafuatia kuundwa kwa mfumo wa kielektroniki (Ankara Jumuishi) utakaosaidia kuimarisha uwazi, ufanisi na tija katika mgawanyo wa mapato yatakayokuwa yamekusanywa kwa kuingizwa moja kwa moja kwenye taasis husika kulingana na asilimia zilizokubalika. Mfumo unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2025.

Wakizungumza katika zoezi la utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo alieleza kuwa mfumo huo wa kielektroniki utarahisisha mgawanyo wa mapato na kuwezesha kila taasis kupata mgao wake kwa wakati ili kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Peter Ulanga amepongeza muitikio kutoka pande zote wa kutekeleza maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mifumo ya taasis za serikali kusomana, naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Daniel Malanga alipongeza hatua iliyofikiwa sababu itaboresha utoaji huduma ndani ya viwanja vya ndege nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a amewashukuru viongozi wenzake kwa kufanikisha kukamilika kwa mfumo huo na kusisitiza kuwa mfumo huo utachangia sana kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kwa kupunguza muda na nguvu kubwa iliyokuwa inatumika kufuatilia mapato yatokanayo na huduma zitolewazo na kila taasis