December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

STAMIGOLD waandaa mpango wa ufungaji Mgodi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wataalam wa Wizara ya Madini wamefanya ziara katika Mgodi wa dhahabu wa STAMIGOLD uliopo wilayani Biharamulo kwa ajili ya kuangalia mpango wa ufungaji wa mgodi huo.

Ziara hiyo imeongozwa na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Mazingira Mhandisi Gilay Shamika.

Mgodi wa STAMIGOLD umeeleza kuwa mpango wa ufungaji wa mgodi upo tayari na unategemewa kupitiwa na Kamati ya Kitaifa ya ufungaji wa migodi mwishoni mwa mwezi Novemba.

Hata hivyo, Kamishna Msaidizi Mhandisi Shamika amewasisitiza kuhakikisha kuwa mpango wao wa ufungaji mgodi unakuwa na taarifa zote zinazotakiwa katika ufungaji wa mgodi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa dhamana ya kurudisha mazingira katika hali yake ya awali inakuwa imewekwa na kuidhinishwa na Kamati ya ufungaji migodi Kitaifa.

STAMIGOLD ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu iliyopo katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.