December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika Ndugai kuzindua ofisi ya TCCIA Makao Makuu Dodoma kesho

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Dodoma

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai anatarajiwa kufungua Ofisi ya Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na kilimo hapa nchini (TCCIA), kama sehemu ya mikakati yake ya kufanikisha utekelezaji wa sera ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa mara baada ya kikao cha ndani cha Bodi ya Wakurugenzi wa Chemba hiyo, Rais wa TCCIA, Paul koyi amesema chemba ni chombo chenye mtandao mkubwa wa wafanyabiasha wenye viwanda na kilimo hapa nchini imejipanga kwenda sambamba na kufanikisha azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.

“TCCIA tayari tumeshaanza kutekeleza azma hiyo ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025 kwa vitendo. Na sasa tunatarajia Spika Job Ndugai atatufungulia ofisi ndogo ya chemba hapa makao makuu ili kuongeza ufanisi wa hazi za chemba,” amesema Koyi.

Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo hapa nchini (TCCIA), Paul Koyi (kulia) akizungumza na wadau, wajumbe wa chemba hiyo mara baada ya kikao cha ndani cha Bodi ya Wakurugenzi ikiwa sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya TCCIA iliyopo Mtaa wa Mazengo jijini Dodoma jana. Kushoto ni mjumbe wa Bodi ya TCCIA, Dkt. Said Kingu na wapili kuchoto ni Dkt, Robert Mashenene mshauri wa TCCIA mkoa wa Dodoma. Katikati ni Ngussa Kinamhala mshauri wa TCCIA na wapili kulia ni mshauri wa TCCIA, Isaac Kissa.

Koyi amesema ufunguzi wa ofisi makao makuu ni mongoni mwa mipango ya TCCIA ya kufanya mageuzi ndani ya chemba ikiwemo ufanisi wa utoaji wa huduma zake kwa wanachama na watanzania kwa ujumla wake.

Amesema TCCIA tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikiteleza majukumu yake kama yalivyoainishwa sambamba kushirikiana na wabia wake kutoka sekta za umma na binafsi katika kuchagiza maendeleo na ustawi wa jamii wakiwepo wanachama wake.

‘’Tunaendelea kutekeleza azma yetu kama TCCIA ya kuwasaidia wafanyabiashara hapa nchini kufikia malengo yao kwa kubeba changamoto zao, mawazo yao na mapendekezo ya nini kifanyike na kuyafikisha kwa wabia mbalimbali hasa wadau toka sekta za umma na kujadili namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara ambayo yataleta tija,” amesema, Koyi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Nebart Mwapwele amesema uzinduzi wa ofisi mpya iliyopo Mtaa wa Mazengo Dodoma utaongeza chachu na ari kubwa kwa wananchama waliopo Kanda ya Kati sambamba na kuziimarisha ofisi za mikoa zilizopo katika mikoa hiyo.

Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo hapa nchini (TCCIA), Paul koyi (katikati) akizungumza kwenye kikao cha ndani cha Bodi ya Wakurugenzi wa Chemba hiyo ikiwa sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya TCCIA iliyopo mtaa wa Mazengo jijini Dodoma itakayofanyika kesho. Kushoto ni mjumbe wa Bodi ya TCCIA, Dkt. Said Kingu na watatu Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Nebart Mwapwele.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo kufika wa wingi kushuhudia uzinduzi wa ofisi yao mpya ambayo itajikita kusikiliza, kubeba mawazo na kuwasilisha changamoto zinazotukabili ili kuweka mzingira rafiki kwa wafanyabiashara,”amesema Mwapwele.

Amesema wanachama pia watapata fursa ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Mazingira wakati wa hafla hiyo muhimu ya uzinduzi wa ofisi ya chemba.