January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Spika achukizwa uzembe kwa viongozi waliokwamisha maendeleo

Na Esther Macha, Timesmajira,Online,Mbeya

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson, amesikitishwa na kitendo cha Halmashauri hiyo pamoja uongozi wa shule ya msingi Iganjo kuchelewesha ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu na matundu ya vyoo 24 ya shule hiyo licha ya yeye kufanikisha upatikanaji wa shilingi Milioni 100 za ujenzi huo.
 
Dkt. Tulia amesema hayo leo wakati alipofanya ziara katika kata ya Igawilo kwa lengo la kuzungumza na wananchi pamoja na kujionea maendeleo ya shule hiyo ambayo siku za karibuni aliombwa kutatua changamoto mbalimbali kwenye shule hiyo ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
 
 “Mzigo huu naitwisha halmashauri, naitwisha kwasababu fedha zinapokuja huku wao ndio watu wa kwanza kupata taarifa na ni kazi yao kuhakikisha shule hizi zinakuwa sawa. Sisi tunatafuta fedha kwa ajili ya kupunguza hizi changamoto za watoto ajabu ni kwamba kazi haifanyiki kwa kigezo eti mchakato, mchakato gani unaofanyika hapa?” amesema Dkt. Tulia.

Aidha Dkt. Tulia amemuagiza Mstahiki Meya wa Jiji hilo kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo na uongozi wa shule wasimamie zoezi la ujenzi huo ndani ya mwezi mmoja kwakuwa ameonesha uzoefu wa kusimamia zoezi kama hilo katika ujenzi wa madarasa ya UVIKO 19 hivyo kwa Imani hiyo ataweza kufanikisha kazi kwa wakati.
 

Kaimu  Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ,Trifonia Kisiga amesema hatua za awali kupitia afisa elimu ilikuwa kumhamisha Mwalimu Mkuu na kufanyika kwa ukaguzi ili ujenzi uendelee.


 
Kwa upande wake Mstahiki Meya, Dourmohamed Issa, amemuhakikishia Dkt. Tulia kwamba atatekeleza hatua hiyo ndani ya muda stahiki ili wanafunzi wa shule hiyo waweze kusoma katika mazingira safi na rafiki.
 
Mmoja wa wananchi wa kata ya Naye ya Igawilo, Aziz Ngole, kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo amemshukuru na kumpongeza Spika Dkt. Tulia kwa maendeleo aliyoyafanya katika kata hiyo pamoja na Jimbo hilo kwa ujumla na kumtaka asiache kuendelea kufuatilia matokeo ya misaada ambayo amekuwa akiitoa.

Aidha Ngole amepinga kitendo cha Halmashauri kutaka kumhamisha Mwalimu Mkuu wa shule Alphonce Mkuchika kwa kile kilichodaiwa kuzorotesha ujenzi kauli iliyoungwa mkono pia na Judith Sungura ambaye alisema Kamati ya ujenzi ndiyo iliyozembea.

Naye Elia Jerema amesema anaitilia shaka Kamati ya ujenzi kwani hata mawe yaliyojengewa msingi hayana kiwango.

Diwani wa Kata ya Igawilo Anna Ndidi amesema yeye hakuwahi kupata taarifa ya maandishi juu ya fedha kupelekwa kwenye shule ya Iganjo kama ilivyo ada lakini baada ya malalamiko ya wananchi aliivunja kamati ya ujenzi.