Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.
KAMISHENI ya pamoja ya bonde la mto Songwe (SONGWECOM) imegawa Ng’ombe 68, wakiwemo mitamba 60 wenye mimba kwa vikundi vinne rafiki wa mazingira katika vijiji vya Ilondo na Bulanga, Wilayani Ileje, lengo likiwa ni kuboresha maliasili ya bonde, pamoja na kuinua hali za maisha kwa wananchi.
Ugawaji wa Ng’ombe hao umefanywa Februari 27, 2024 katika kijiji cha Ilondo na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Ileje, John Komba, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Frida Mgomi.
Akizungumza kabla ya zoezi la kukabidhi Ng’ombe hao kufanyika, Ofisa Utawala,Uratibu na Manunuzi kutoka Kamisheni hiyo, Ghoyela Mpangala, ambaye alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Kamisheni hiyo, Dkt. Mhandisi Ladislaus Kyaruzi, alisema kuwa mradi huo wa ngombe wa maziwa walionunuliwa kwa thamani ya shilingi milioni 130 umefadhiliwa na mfuko wa dunia wa Mazingira (GEF) kupitia benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB).
“Ndugu mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Ng’ombe hawa wamenunuliwa kutoka katika shamaba la serikali la Sao hill lililopo mkoani Iringa, amabapo kati ya hao 68, mitamba ni 60 kwa ajili ya miradi ya maziwa kwa wanufaika, yakiwemo madume nane kwa ajili ya kupandishia,”amesema Mpangala.
Mpangala amesema kuwa, Kamisheni hiyo ya pamoja ya Bonde la mto Songwe iliyoundwa na nchi za Tanzania na Malawi, ilianza shughuli za utekelezaji wa miradi ya ngazi ya jamii katika Wilaya mbili za Ileje nchini Tanzania, pamoja na Wilaya ya Chitipa nchini Malawi.
“Mradi huu mbali na kulenga kuwaongeza kipato wananchi wa vijiji hivi, unalenga pia kuboresha na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji na ardhi katika maeneo yao,”amefafanua Zaidi Mpangala.
Aidha,amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi huo kuhakikisha wanausimamia mradi huo na kuwa endelevu kupitia mfumo wa kopa Ng’ombe lipa Ng’ombe ili kuhakikisha kuwa wananchi wote walio ndani ya bonde la mto Songwe wananufaika na mradi unatimiza malengo yakeya kuboresha kipato na lishe huku mazingira yakihifadhiwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Komba ameishukuru Kamisheni ya pamoja kwa mradi huo, huku akitoa wito kwa kuwataka wananchi kuwatunza Ng’ombe hao kutokana na maelekezo ya wataalam.
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ubatizo Songa na Nuru Kindamba, waliwasihi wanafaika mradi huo kuhakikisha wanatunza Ng’ombe hao ili wananchi wengine nao waje kujifunza kutoka kwao.
Bonde la mto Songwe lenye ukubwa kilometa za mraba 4,243 linajumuisha wilaya saba za mataifa mawili ya Tanzania na Malawi ambazo ni Ileje, Mbeya Vijijini, Momba, Mbozi na Kyela nchini Tanzania, wakati Kalonga na Chitipa zikiwa upandfe wa Malawi.
Pia mto Songwe ni sehemu ya mpaka wa Tanzania na Malawi wenye urefu kilomita 200, ambapo bonde linalohifadhi uhai wa mto huo likiwa linakaliwa na wakazi 314,104 kwa mujibu wa tathimni zilizofanyika.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa