Na Moses Ng’wat,TimesMajira Online. Songwe
HALMASHAURI ya Wilaya ya Songwe kupitia Idara za Elimu Msingi na Sekondari, zimeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na wimbi la wanafunzi wanaokatisha masomo ‘mdondoko’ na tatizo la mimba kwa wanafunzi.
Hayo yamesemwa na Ofisa Elimu Shule ya Msingi, Michael Nzunda wakati akizungumza na Majira kuhusiana na mikakati ya halmashauri, kukabiliana na wimbi la wanafunzi wengi kuacha shule na kujiingiza katika shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu, ufugaji na uvuvi wilayani hapa.
Amesema licha ya jamii na wadau wengi wa elimu kuamini kuwa uwepo wa migodi ya uchimbaji wa dhahabu, shughuli za ufugaji na uvuvi ndiyo sababu zinazosababisha wanafunzi kuacha shule.
Nzunda amesema mbali na sababu hizo, bado kuna sababu nyingine kama majanga ya asili ama mafuriko kwa namna nyingine, yamekuwa yakichangia kuwepo kwa tatizo la wanafunzi kukatisha masomo.
Amesema halmashauri hiyo ambayo jiografia yake kwa sehemu kubwa ni bonde linalopokea maji kutoka Mikoa ya Mbeya na Tabora kwa ajili ya kuingia Ziwa Rukwa, hukumbwa na mafuriko na kuvitenganisha vijiji hali inayosabibisha baadhi ya wanafunzi, kushindwa kuhudhuria masomo kwa muda mrefu na baadaye kukata tamaa na kukimbilia mitaani.
Ofisa huyo amesema katika kukabiliana na sababu hiyo, tayari halmashauri imejenga jumla ya shule shikizi 29 kwa ajili ya kunusuru wanafunzi ambao shule zao, zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya mafuriko.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari, Steven Bange ametaja miongoni mwa mikakati inayochukuliwa kudhibiti tatizo la wanafunzi kukatisha masomo ni baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika familia duni, kupewa ufadhili kutoka kwa wadau wa elimu.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019 hadi 2021, jumla ya wanafunzi 739 walikatisha masomo yao.
Bange amesema sababu kubwa za wanafunzi hao kuancha masomo na kusababisha mdondoko ni kujiingiza kwenye shughuli za uchimbaji wa dhahabu, ufugaji na uvuvi pamoja na wanafunzi wa kike kupewa ujauzito.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best