January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Songwe waomba kutatuliwa kero ya maji

Na Esther Macha,TimesMajira Online. Mbeya

WAKAZI wa Kata ya Imalilo Songwe wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya, wameiomba serikali kuwatatulia kero ya maji inayowakabili kwa muda mrefu sasa na kushindwa kupata huduma ya maji safi na salama.

Baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamesema, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji kwa zaidi ya miaka 20, hivyo hushindwa kupata huduma ya maji ili kuweza kukidhi haja zao.

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa wakazi wa Kata ya Imalilo Songwe, Theresia Juma amesema kutokana na shida hiyo ya maji imekuwa ikiwalazimu kwenda kuchota maji ya visima na wakati mwingine, kununua maji kwa bei ghali ambayo hutoka ubaruku ili kuweza kutumia.

Habakuki Daimoni ambaye ni Mwenyekiti wa Imalilo Songwe, amesema kumekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu ambayo inawasababishia wazazi wa eneo hilo, kushindwa kupata huduma ya maji kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

“Hili kwetu ni tatizo kubwa sana, tunaomba serikali itusaidie kuona changamoto hii ya maji,” amesema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Imalilo Songwe, Consolata Mapunda amesema maji yamekuwa yakisumbua kwa muda mrefu sasa hivyo wamefanya jitihada za kuweza kuhakikisha wananchi, wanapata maji safi na salama kwa kuahidiwa na Mkuu wa Mkoa kuwaletea maji katika kata hiyo.

Amesema jitihada bado zinafanyika, ili kuhakikisha kuwa wananchi wa kata hiyo wanapatiwa maji.