Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa elimu haina mwisho na ni suala mtambuka ambalo ni kipaumbele cha kwanza ulimwenguni kote.
Wito umetolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi katika shule ya msingi Juhudi iliopo Kata ya Kiseke wilayani Ilemela mkoani Mwanza, wahakikishe watoto hao wanaendelea na masomo ya sekondari ili kutimiza ndoto zao.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) Edwin Soko aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)Kenneth Simbaya,katika mahafali ya kuwaaga wahitimu wa darasa la saba wa shule ya msingi Juhudi yaliofanyika shuleni hapo.
Soko ameeleza kuwa,wazazi wasikatishe masomo kwa watoto hao kuacha kuendelea na elimu ya sekondari kwa kuwaozesha mabinti zao huku wakiume wasiachishwe kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nyingine.
Pia ameeleza kuwa vitendo vya ukatili vinaongezeka na takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa watoto wanafanyia na watu wao wa karibu,hivyo ni jukumu la kila mmoja kuwalinda.
“Umri wa kazi na kuolewa utafika,tunahitaji watoto hawa waendelee na masomo kama wazazi tuzingatie hilo,lakini kwa wakati huu ambao tunasubili matokeo yao tuepuke manyanyaso ya kijinsia kwa watoto wetu pande zote mbili matendo ambayo yatawaathiri kimwili,kiakili na kiroho,”ameeleza Soko.
Mbali na hayo Soko amewahimiza wazazi kupunguza utoaji michango katika harusi na badala yake waelekeze katika kutatua changamoto zilizopo shuleni ili kuweka mazingira bora ya kusoma na kufundishia.
“Tusisubili serikali kuwa itafanya kama wadau tukiziacha changamoto hizi zitarudisha nyuma maendeleo ya watoto wetu, UTPC itachangia kiasi cha milioni 1 kwa ajili ya ununuaji wa mashine ya kuchapishia majaribio printer pia kama waandishi tutahakikisha inapatikana uzio kupitia changizo ili kuwalinda watoto,”ameeleza Soko.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi mmoja wa wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi Mariam Faraja,shule hiyo ilianza na wanafunzi 572 kwa sasa ina wanafunzi 1144 huku waliohitimu elimu ya msingi kwa mwaka huu ni 141.
Mariam ameeleza kuwa changamoto katika shule hiyo ni ukosefu wa mashine ya kutolea chapa kwa ajili ya mitihani,ukosefu wa Umeme,vifaa vya tehama,upungufu wa vyumba vya madarasa kwani mahitaji ni madarasa 29 yaliopo ni 11 upungufu ni 18.
Madawati mahitaji 412 yaliopo 311 na upungufu ni 101, ukosefu wa vifaa vya michezo huku wakitoa mapendekezo kwa wadau kuomba wawasaidie kutatua changamoto zilizopo katika shule hiyo ili wanafunzi waweze kufanya majaribio ya mara kwa mara na kuwasaidia kufanya vizuri kitaaluma.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya msingi Juhudi,Manyasi Magai, ameeleza kuwa changamoto kubwa ni shule hiyo kutokuwa na uzio na ipo barabarani ambayo inaweza kusababisha kushindwa kuwamudu watoto kwani wanaweza kutoroka wakati wote.
“Kukosekana kwa uzio kumechangia ajali mfano mwaka huu tangu umeanza tumepata ajali nne za wanafunzi wetu kati yao mmoja alifariki,tunawashukuru wadau waliojitokeza kusaidia kutatua changamoto hizi,serikali imekuwa ikipambana kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kufundishia na ufundishwaji,”ameeleza Mwl.Magai.
Naye mdau wa maendeleo, Mkurugenzi Mtendaji wa Rek One Co.LTD Mhandisi Elius Rwegasila, ameeleza kuwa shule hiyo ina changamoto mbalimbali na wao kama wadau kupitia kampuni yao wanaunga mkono juhudi za serikali katika utoaji wa elimu ambapo wataweka mfumo wa umeme kwa madarasa yote katika shule hiyo.
Pamoja na kuunganisha umeme ili mwanga upatikane ambao utasaidia wanafunzi kusoma wakati wote na kuimarisha ulinzi kwani wahalifu wanajificha katika giza.
“Kama sehemu ya hamasa kampuni yetu tutajitoa kuwashika wanafunzi watakaoshika nafasi ya tatu bora kila mwaka kwa kutoa kiasi cha 50,000, katika mitihani kwa darasa la tano na sita,ili kuwafanyia wanafunzi kufanya vizuri na tutaongea na wadau wengine ili kuboresha zawadi hizo ili walimu watakaokuwa bora wapate zawadi,”ameeleza Mhandisi Rwegasila.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi