December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Sio sheria zote za habari zenye ukakasi’

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

IMEELEZWA kuwa ni wakati mzuri kwa mabadiliko ya sheria kwa kuwa rais aliyepo madarakani ameonesha dhamira ya mabadiliko hayo.

Hayo ameyasema James Marenga, wakili wa kujitegemea wakati akizungumza katika Kituo cha Radio Tumaini (Tumaini FM), jijini Dar es Salaam kuhusu mwanya ulipo kwenye sheria za habari na hatari yake.

“Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10. Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele,” amesema Marenga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania (MISA TAN).

Wakili Marenga amesema wanaamini sheria hizo na zingine ambazo wameorodhesha kwenye nakala yao ya mapendekezo ya mabadiliko, wadau na serikali kwa pamoja watapitia na kuona namna ya kunyoosha ili mapendekezo hayo yatapopelekwa bungeni, wawe na msimamo unaofanana.

Kwa upande mwingine Wakili marenga amesema endapo mwandishi ataandika habari ambayo italeta taharuki kwa wananchi na kusababisha kuichukua serikali yao, haijalishi ukweli wake, kwa mujibu wa sheria za habari zilizopo, atakuwa ametenda jinai.

“Sheria inaelekeza kwamba, kama mwandishi ataandika habari ambayo itawasisimua wananchi na kupandwa na hasira licha ya ukweli wa habari hiyo, sheria inasema atakuwa ametenda jinai.

“Kwa mfano; mwandishi akifanya uchambuzi kuhusu njaa, upandaji wa mafuta, upungufu wa maji ama kukosekana kwa mkate na habari ile ikasababisha hasira kwa wananchi, inaweza kumgharibu. Sheria inasema lazima apate kibali kutoka serikalini,” amesema Wakili Marenga akiwakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika mazungumzo hayo.

Kwa upande wake Mhariri wa Gazeti la Mwananchi Rashid Kejo, amesema, sio sheria zote za habari zenye ukakasi, bali kuna maeneo yanayoibua sintofahamu hivyo wadau wa habari wameomba kuangaliwa upya.

“Mchakato huu wa mabadiliko ya sheria, haulengi kung’oa sheria zote kwa kuwa, zipo nzuri na zenye maana kubwa katika tasnia ya habari, mfano kulazimisha maofisa wa serikali kutoa taarifa kwa waandishi, kutambua maslahi na mikataba ya waandishi, mambo mazuri, yapo mengi,” amesema Kejo.

Ameeleza kuwa, Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, ina maeneo ambayo yanazuia kukuwa kwa tasnia hiyo akitoa mfano sheria aliyopewa Mkurugenzi wa Habari Malelezo ya kupeleka matangazo kule anakojisikia.Taasisi zote zimeelekezwa kupeleka matangazo Habari Maelezo, ambao mkurugenzi wake ndiye atayeamua chombo cha habari cha kutangaza.

“Serikakli ndio mtangazaji mkubwa, sasa chombo kitachoonekana kukosoa serikali bila shaka kitakosa matangazo, hapo ni kuua kazi ya uanahabari lakini pia kuua uchumi wa wanahabari.

“Lakini pia, tasnia ya habari inahitaji uwekezaji mkubwa, sheria yetu inambana mwekezaji wa nje ya nchi kuwekeza kwa asilimia 100, ametakiwa sizidi asilimia 49 tu, huku ni kufanya tasnia idumae. Tunatamani haya yote yabadilishwe,” amesema Kejo.