December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba:Uzembe sekta ya fedha ,kuhujumu fedha za Serikali

Na Mwandishi Wetu,Arusha

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, amesisitiza umuhimu wa taaluma ya ununuzi na ugavi kama msingi wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini, huku akiwataka wataalamu katika sekta hiyo kutokuwa nyuma katika kuongeza weledi na ubunifu.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (APSP) uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Bw. Simba aliipongeza APSP kwa jitihada zake za kuboresha taaluma hiyo na kusisitiza kwamba suala la uzembe katika sekta ya ununuzi halikubaliki na kwamba linaweza kuhujumu thamani ya fedha za serikali kwenye miradi ya maendeleo.

“Taaluma ya ununuzi na ugavi ni mhimili wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini. Ukosefu wa weledi unaweza kusababisha miradi hiyo kutekelezwa chini ya kiwango, jambo linaloathiri maendeleo ya taifa,” amesema Bw. Simba.

Aidha, Simba amewataka wataalam wa ununuzi kubadili mtazamo wao na kutumia mifumo ya kisasa kama Mfumo wa Kielektroniki wa NeST, akisema kuwa mfumo huo umewekwa ili kuhakikisha uwazi na usawa katika ununuzi wa umma.

“Hakuna nafasi ya ‘connection’ katika ununuzi wa umma. Mfumo wa NeST unahakikisha kila hatua inafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria,” aliongeza Bw. Simba huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka sheria.

Mwenyekiti wa APSP Bw. Emmanuel Urembo amesema ameishukuru PPRA kwa kutambua nafasi ya Chama hicho sambamba na kuona umuhimu wao katika sekta ya Ununuzi ambapo ameahidi kutoa ushirikiano wa kujadili hoja za kitaaluma katika sekta hiyo nyeti nchini ili kuibua uibua mambo yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la Ununuzi.

“Na sisi tumejipanga kuhakikisha tunajadili hoja za msingi zitakazokuwa Masada kwenye nchi yetu” Amesema Bw. Urembo

Kwa upande mwengine. Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa amesema kuwa katika nyakati tulizonazo sasa msaada wa kiutendaji sambamba na kutoa suluhisho ya matatizo ni muhimu zaidi kuliko kujifunza na kutoa mawazo ya kufikirika.

“ Natamani watoa mada wetu hapa mjikite zaidi katika kufundisha vitu vinavyosaidia jinsi ya kupambana na changamoto tulizonazo katika sekta yetu kuliko kutumia muda mrefu kufundisha mawazo ya kufikirika” Amesema Nyaisa

Katika hatua nyingine, Bw. Simba aliahidi kuwa PPRA itachangia Shilingi Milioni 25 kusaidia ununuzi wa kiwanja cha APSP jijini Dodoma, huku akiwasihi wanachama wa chama hicho kushirikiana kufanikisha ndoto hiyo.

Mkutano huo ulijadili mada mbalimbali zinazohusu kuboresha mnyororo wa thamani wa ununuzi na ugavi kwa maendeleo ya taifa ukihusisha zaidi ya wataalamu 150, kutoka kada ya Ununjuzi na Ugavi kutoka maeneo mbalimbali nchini kuhusu kaulimbiu ikiwa ni “Taaluma, Thamani na Kujenga Uwezo”