Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Siku 365 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani,ameipatia Wilaya ya Ilemela kiasi cha zaidi ya bilioni 3 kwa ajili ya kupima,kurasimisha,kupanga mji na kumilikisha ardhi.
Hiyo ikiwa ni jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha inapunguza na kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi kwa Wilaya hiyo na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya siku 365 za Rais Samia kwa Wilaya ya Ilemela,iliofanyika wilayani humo mkoani Mwanza, Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amesema,Ilemela ni moja ya halmashauri 55 zilizokidhi vigezo kati ya 78 zilizoomba fedha kwa ajili ya zoezi hilo la upimaji wa ardhi,urasimishaji na umilikishaji.
Dkt Angeline amesema,wilaya hiyo imepata bilioni 3.58 za kupima ardhi,kumilikisha,kurasimisha,kupanga na kupendezesha mji na hivyo kuondoa migogoro ya ardhi na ujenzi holela.
“Rais Samia amekuja na tiba ya migogoro ya ardhi inayosababishwa na kutopima ardhi na kuimilikisha,kwani bila kupima na kumilikisha unaleta migogoro,tunapopima ardhi hatutaki watu waondoke,wapo watakaobaki sababu wanaendesha maisha yao kwa kilimo,”amesema Dkt Angeline.
Amesema,mpango huo utawapeleka kwenye hatua kubwa zaidi na kuimarisha shughuli za uzalishaji za wananchi kwa kutumia ardhi hiyo kwa kilimo na ufugaji pamoja na kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa kero ya muda mrefu.
“Tunasema ahsante Rais Samia kwa kutuwezesha kwa kiwango kikubwa Ilema Ina asilimia 90 ya upimaji viwanja kwa Jimbo la Ilemela na ndani ya muda mfupi tunafikia asilimia 100,hivyo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela zisimamieni vizuri fedha hizi, zitumike kuleta matokeo chanya kwa kupunguza na kuondoa uendelezaji na ukuaji holela wa miji,kupendezesha mitaa na kuongeza maeneo ya ardhi ya akiba na miundombinu ya kijamii na kiuchumi,” amesema Dkt.Angeline.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mhandisi Modest Apolinary, amesema fedha hizo zitawawezesha kuendeleza ardhi na kupima viwanja ambapo wanapima zaidi ya viwanja 2,000 na sasa wamefikia zaidi ya asilimia 50.
“Tumepata kiasi cha bilioni 3.56 ili kuendeleA ardhi yetu na eneo tunalolilenga ni ya Ukanda wa Ziwa letu sasa tumefika zaidi ya asilimia 50,hivyo wananchi mkae tayari tutangaza kwa wale wanaopenda kuwekeza katika eneo hili kwa kujenga hoteli,viwanda na hata Makazi waje kupata viwanja kwa bei nafuu,”amesema.
Mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Ilemela waliohudhuria hafla hiyo Minza Mayala,ameipongeza serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zitawezesha kupanga na kuendeleza miji na vijiji ambacho ni kipaumbele cha wizara hiyo.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM