November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sikonge yatoa chanjo ya mapele kwa Ng’ombe 14,000

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imeendelea kutekeleza zoezi la ustawishaji mifugo kwa kutoa chanjo ya kudhibiti ugonjwa wa mapele kwa jumla ya ng’ombe 14,000 katika kata 4, zoezi hili linaendelea katika kata zote.

Akizindua zoezi hilo jana Mkuu wa Wilaya hiyo Cornel Magembe amesema kuwa zoezi hilo ni muhimu sana kwa kuwa litasaidia kustawisha mifugo inayozalishwa na wafugaji katika vijiji na kata zote za Wilaya hiyo.

Amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka 2 zoezi hilo limekuwa likifanyika katika Wilaya nzima na limekuwa na matokeo chanya yaliyopelekea kuongezeka kwa mifugo ikiwemo kudhibitiwa ugonjwa huo uliokuwa ukipoteza ng’ombe wengi.

Ili kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa katika vijiji vyote ametoa wito kwa wafugaji wanaoficha mifugo yao kuacha mara moja tabia hiyo huku akiagiza Viongozi wa Serikali za Vijiji na Watendaji wa Kata kutoa taarifa ya watu wa namna hiyo.

‘Yeyote atakayebainika kuficha mifugo au kukwamisha zoezi hili kwa namna yoyote ile atachukuliwa hatua kali za kisheria, tunataka mifugo yote ipate chanjo hii na magonjwa mengine yadhibitiwe pia’, amesema.

Naye Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo Maulid Rajabu amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 walichanja jumla ya ng’ombe 99,303 na kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wamefanikiwa kuchanja jumla ya ng’ombe 112,116.

Ameshukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuwezesha Wilaya hiyo kujenga majosho 18 na kuwaongezea kiasi kingine cha sh mil 92 kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuongeza majosho mengine 4 hivyo kuwa na majosho 22.

Aidha amebainisha kuwa halmashauri hiyo pia imeendelea kunufaika na dawa za ruzuku zinazotolewa na serikali kila mwaka ambapo kwa mwaka 2023/2024 wamepata mgao wa dawa aina ya rol-dip lita 129 za kuogeshea mifugo ili kudhibiti kupe.

Akiongea kwa niaba ya wenzao, mfugaji Mao Maganga mkazi wa kata ya Ngoywa Wilayani humo ameishukuru serikali kwa kuwaletea chanjo hiyo kwani mifugo yao ilikuwa inakufa ovyo wakiwa porini bila kujua ugonjwa unaowaua.