December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siasa za machafuko hazikubaliki nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

SIASA zenye dalili za kuleta machafuko nchini Tanzania zinapaswa kupigwa marafuku kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walikamatwa na Polisi jijini Mbeya kwa kukiuka zuio la kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa chama hicho.

Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake David Misime lilieleza sababu ya kuzuia kongamano hilo katika kipindi hiki ambacho mikutano ya siasa imeruhusiwa kuwa ni kauli za kichochezi za viongozi wa Chadema wakitaka Tanzania iwe kama Kenya, ambayo imekumbwa na machafuko makubwa ya kisiasa yaliyojeruhi mamia ya wananchi na wengine wakipoteza maisha.

Tofauti na Kenya, jamii ya Watanzania imeshajipambanua kama wapenda amani na maridhiano, jambo ambalo limeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa wa amani na utulivu barani Afrika na duniani kote – miaka na miaka. Changamoto kubwa katika historia ya Tanzania, ikiwemo kupigania uhuru, zilitatuliwa bila kumwaga damu.

Amani na Utulivu umeiwezesha nchi ipige hatua kubwa za kimaendeleo ambazo yasingewezekana kama Taifa lingekuwa kwenye machafuko. Kutamani machafuko na umwagaji damu unaondelea nchini Kenya utokee Tanzania, ni jambo linalopaswa kukemewa kwa nguvu zote.

Toka aingie madarakani, Rais Samia amekuwa akihubiri maridhiano na umoja wa kitaifa na ameitekeleza kwa vitendo falsafa yake ya 4R kwa kuruhusu mikutano ya siasa, kushiriki mkutano wa Chadema.
Hakuna Rais mwingine wa Tanzania amewahi kufanya sanjari na kuweka mazingira ya usalama na ustahimilivu wa kisiasa ambao yamepelekea wanasiasa wa upinzani kama Tundu Lissu na Godbless Lema kurudi nchini kuendelea na shughuli zao za kisiasa kwa uhuru mkubwa.

Hata hivyo, 4R za Rais Samia hazimaanishi kuruhusu fujo na uhuni wa kisiasa unaoweza kuliingiza Taifa kwenye machafuko. Chadema wamefanya mikutano ya siasa zaidi ya 40 na maandamano kwenye majiji yote makubwa nchini, lakini wameshindwa kuwashawishi Watanzania kuwaunga mkono kwa kiwango walichotarajia.

Baada ya kuona wameshindwa kwenye ulingo wa siasa za kistaarabu, sasa wamechagua siasa za machafuko. Watanzania hawaungi mkono machafuko, na Jeshi la Polisi lina jukumu la kulinda amani na usalama nchini.