March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Beyond School Academy kuleta mapinduzi ya elimu kwa njia ya kidigitali,wazazi watakiwa kuchangamkia fursa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira

KATIKA maonesho ya  Sabasaba mwaka huu, shule ya Beyond ‘Beyond School Academy ‘imeibuka kama miongoni mwa taasisi za elimu zinazotumia teknolojia ya kisasa kuleta mapinduzi makubwa katika mfumo wa utoaji elimu nchini.

Akizungumza katika banda la shule hiyo, Bi. Gloria Mbawile, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Beyond School Academi, amesema jukwaa hilo la kidigitali linawalenga wanafunzi wa shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, likiwa na lengo la kumpa mwanafunzi fursa ya kusoma bila kikomo cha mahali wala muda.

“Siyo lazima mtoto awe darasani ili apate elimu. Mtoto anaweza kujifunza akiwa nyumbani, akiwa likizo, au popote pale alipo. Tunawapelekea watoto elimu kiganjani,” alisema Bi. Mbawile.

Kupitia tovuti yao www.beyondschool.co.tz, wanafunzi hupata masomo ya mtaala wa TAI kwa njia ya video, mihadhara ya moja kwa moja (live classes), pamoja na maudhui mengine ya kujifunzia ambayo yanaweza kufikiwa kwa kutumia simu, kompyuta mpakato (laptop), au hata projecta kwa mazingira ya darasa la nyumbani.

Bi. Mbawile alisema kuwa jukwaa hilo pia limezingatia usalama wa watoto kwa kuhakikisha wanafunzi wanaweza kujifunza katika mazingira salama bila hofu ya kukutana na changamoto za kimalezi au ukatili ambazo mara nyingine huwapata wanapokwenda kusoma masomo ya ziada maeneo mbalimbali.

“Mtoto anaweza kujifunza akiwa nyumbani, huku mzazi akiwa na amani. Ikiwa mzazi ana wasiwasi kwamba kifaa cha mwanawe kinaweza kutumika vibaya, sisi tunasaidia kufunga programu zote nyingine na kubakisha ya masomo pekee,” alieleza.

Mbali na hilo, mfumo huo huruhusu mwanafunzi aliyekwama kuelewa somo au mada fulani kuwasiliana moja kwa moja na walimu kupitia Google Meet, hivyo kupata ufafanuzi wa papo kwa papo jambo linaloimarisha uelewa wa mwanafunzi na kuongeza ubora wa elimu anayopata.

Bi. Mbawile ametoa wito kwa wazazi kuchangamkia fursa hii kwa kuwaandikisha watoto wao katika shule hiyo ya mtandaoni, akisema kuwa hiyo ndiyo njia ya kisasa na salama ya kuwasaidia watoto kupata elimu bora bila gharama kubwa au changamoto za kusafiri umbali mrefu.

“Kupitia Beyond School Academy , tumepunguza changamoto nyingi watoto hawalazimiki kusafiri kwenda mbali kwa ajili ya masomo ya ziada ‘tuition ‘, wanajifunza kwa amani, na wanapata msaada wa moja kwa moja kutoka kwa walimu. Hii ni elimu ya kisasa kwa mtoto wa sasa,” alisisitiza.